MUNGU WETU NI MOTO ULAO WAEBRANIA 12:29.

Sunday, May 31, 2020

VIWANGO VYA KUMTAFUTA MUNGU

Na Bishop Dankton Rudovick Rweikila

31st May 2020
2 Nyakati 20:20
Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini Bwana, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.

Maana ya kumuamini Mungu ni ili uweze kudhibitika mahali. Mungu anakudhibitisha kwamba Baraka hizi ni za kwako na mafanikio haya ni ya kwako kwenye ulimwengu wa Roho lakini mafanikio hayatokei pasipo kuamini watumishi wa Mungu. Unapoambiwa piga kelele maana yake kupiga kelele ndiyo kufanikiwa kwako kulipo. Mafanikio yako yanadhibitika unapoamini watumishi wa Mungu na hapo utayaona yakitokea.

Yesu alitenda miujiza kwasababu walimuamini Mungu na walimuamini Yesu, shida ya leo watu wanamuamini Mungu lakini awaamini watumishi wa Mungu. Yesu aliwaambia wale wakoma kwamba waende wakijionyeshe kwa makuhani. (Luka 17:14) Dalili za uponyaji wako amebeba mtumishi wa Mungu na akikuambia kwamba umepona amini kwamba umepona.

Yesu anafika kwa Lazaro anawaambia waondoe jiwe na walisema ananuka lakini aliwaambia waondoe jiwe (Yohana 11:1-45).  Wengi wanapoambiwa wamepona au watafanikiwa shida inakuwa kuwaamini watumishi wa Mungu.

Jambo lilitokea kwa wana wa Israeli na Debora nabii alimuambia Mungu amewashindia kwa Sisera aliyewatesa. Mfalme akasema yeye hawezi kwenda peke yake bila yeye, Sisera aliyetesa taifa anakufa kwenye mikono ya kibibi tu. Nabii Deborah alikuwa akitembea kawaida lakini Malaika wa Bwana walikuwa wakimkimbiza Sisera na magari yake. Deborah alimuambia Mfalme nikienda na wewe utukufu hautakuwa kwako bali Mungu atajitwalia utukufu kwa mwanamke mmoja. Walipoamini maneno ya Deborah ndipo Mungu aliwatetea na kuwasaidia. (Waamuzi 4:1-24)

Najua unamwamini Mungu lakini amini na watumishi wako ili uthibitike, na mimi natamka kwenye maisha yako hautabaki kama ulivyo kwa jina la Yesu.

Ayubu 20:15
Amemeza mali, naye atayatapika tena; Mungu atayatoa tumboni mwake.

Mungu anajua kwamba yupo aliyemeza mali lakini yeye amesema aliyemeza atayatapika na yeye peke yake atayatoa kwenye tumbo lake. Unaweza kuwa na watoto wakamezwa, unaweza kuwa na ndoa ikamezwa lakini sikia Bwana ataitoa kwenye matumbo yao leo.

Mithali 16:3-7
Mkabidhi Bwana kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika. 4 Bwana amefanya kila kitu kwa kusudi lake; Naam, hata wabaya kwa siku ya ubaya. 5 Kila mwenye moyo wa kiburi ni chukizo kwa Bwana; Hakika, hatakosa adhabu. 6 Kwa rehema na kweli uovu husafishwa; Kwa kumcha Bwana watu hujiepusha na maovu. 7 Njia za mtu zikimpendeza Bwana, Hata adui zake huwapatanisha naye.

Kiburi kinakufanya ujisikie kwamba wewe ni muhimu kuliko mtu mwingine. Katika Biblia tunamuona Mordekai ambaye alikuwa ni mtu wa kawaida aliyekaa kwenye malango ya mfalme lakini aliposikia habari za mfalme kutaka kuuliwa alikimbia na kutoa habari za kuokoa maisha ya mfalme (Esta 2:21-23).  Kiburi hakifai kwasababu tunategemeana. Kuna mtu ambaye unamdharau lakini nikuambie unaweza kuwa unaishi kwa niaba yake. Mtu mmoja alipata nafasi na akatizama mke wake na kumuambia kwamba sasa hivi unifai kwasababu ya nafasi aliyokuwa ameipata. Lakini yule mama akamwambia kama nikitoka kwenye maisha yako jua kwamba utakosa hiyo nafasi na akasema umeipata kwasababu yangu.

Mithali 26:27
Achimbaye shimo atatumbukia mwenyewe; Naye abingirishaye jiwe litamrudia.

Kuna watu wanachimba mashimo kwaajili yako ili wakuweke humo. Na leo tunakataa mashimo hayo katika jina la Yesu na mashimo waliochimba tutawadumbukiza wao katika jina la Yesu.

Wako watu ambao wanapanda mabaya kwenye maisha yako kwasababu ya siku ya ubaya, wanachotamani ni kumeza maisha yako, mtaji wako na familia yako kwa ujumla ili uingie kwenye mashimo. Adui akishakuweka kwenye shimo anahakikisha kwamba amekufunika. Wakichimba shimo wanaweka jiwe juu yako na kukufunika ili wewe usitoke. Umewekwa kwenye umasikini na wamekuwekea jiwe la umasikini kama kifuniko ndiyo maana kila ukitaka kutoka hapo hauwezi kwasababu umasikini unakufuata. Lazima tuviringishe jiwe ili shimo hilo litoke kwenye maisha yako. Lazaro alipokufa waliweka jiwe juu yake na Yesu akawaambia waondoe jiwe kwasababu bila kuondoa jiwe Lazaro asingeweza kutoka. Malaika walipokwenda kaburini kwa Yesu chakwanza walichofanya ni kuviringisha lile jiwe na walipomaliza walilikalia. Na leo ninaamuru Malaika waviringishe jiwe la umasikini kwenye maisha yako na kulikalia kwa jina la Yesu.


Shetani anajua umewekwa kwenye hali ya uharibifu lakini anakuwekea jiwe la uovu, na anajua umewekwa kwenye hali ya kutofanikiwa kwa kila utakachofanya sasa anakuwekea jiwe la kutotoa fungu la kumi.

Ili ushinde adui yako lazima uhakikishe lile jiwe waliloviringisha kwa ajili yako linawarudia wao.

Tembelea Youtube yetu pamoja na Facebook account zetu za Power of God Fire Church. 

No comments: