MUNGU WETU NI MOTO ULAO WAEBRANIA 12:29.

Tuesday, January 23, 2018

Utii wa Mke

submissive
Efeso 5:22-23 Wake, watiini waume zenu kama mnavyomtii Bwana. 23Kwa maana mume ni kichwa cha mke kama vile Kristo alivyo kichwa cha kanisa, ambalo ni mwili wake, naye mwe nyewe ni Mwokozi wa kanisa.
Biblia inamwagiza mke kuwa mtii kwa mume wake kama kwa Kristo kwa maana mume ndiye kichwa cha nyumba. Utii huu wa mke kwa mume kwa lugha ya kiingereza wanasema ‘submission’ yani kukubali kwa hiyari kujitoa kuwa chini ya uongozi wa mume wako. Kumfanya mume kuwa ndiye kiongozi wa nyumba yako na wewe kwa unyenyekevu kukubali kufuata uongozi huo. Utii huu unajengwa na upendo na heshima uliyonayo kwa mume wako.
Utii huu wa kibiblia wa mke kwa mume haumaanishi kuwa mke anakuwa hana maamuzi wala nafasi ya kutoa mawazo yake, wala haimaanishi kuwa mke afanye kila mume analomwambia bila kulipima na neno la Mungu na wala sio kuwa mume ni bora mbele za Mungu kuliko mke, bali mke kukubali kuwa chini ya uongozi wa mume, kumshirikisha mambo yote kabla ya yeye kufanya maamuzi na kumweka mume wake (pamoja na mahitaji ya mume wake) kuwa ni muhimu kuliko yeye.
Wafilipi 2:3 Msifanye jambo lo lote kwa ajili ya ubinafsi au kwa kujiona, bali kuweni wanyenyekevu, mkiwahesabu wengine kuwa bora kuliko ninyi.
Kitabu cha mithali 31:12 biblia inaonyesha kuwa mke mwenye utii atakuwa anamtendea mumewe mambo mema siku zote. Atakuwa bega kwa bega na mume wake katika mambo yote bila kutarajia malipo yoyote bali atafanya hivyo ili kumpendeza mume wake na kumpa Mungu utukufu. Ndoa ikikosa utii wa mke mara nyingi hukumbwa na migogoro ya mara kwa mara. Haijalishi nani ana kipato zaidi ya mwingine bado nafasi ya mume kama kichwa inabaki pale pale.
Moyo wa mume unahitaji kukubalika na mkewe, kuheshimiwa na zaidi ya yote upendo usio na mipaka. Hata kama atapata upendo na heshima toka kwa ndugu na jamaa  na akakosa toka kwa mke wake mume huyo atakuwa ni mtu asiye jiamini na mnyonge na matokeo yake atashindwa kufanya kazi zake kwa ufanisi au atakuwa ni mtu mwenye hasira mara kwa mara. Heshima toka kwa mke ndio nguvu kubwa ya kumfanya mume kuwa na ujasiri wa kukabiliana na maisha yake.
Ili mke aweze kuwa mtii kwa furaha bila kuona shida wala kulazimishwa, mume anapaswa kujua jukumu lake la kumpenda mkewe kama Kristo alivyolipenda kanisa na kuwa tayari kufa kwa ajili  ya kanisa. Huu ni upendo mkuu wa kumpenda mke kuliko nafsi yako na kumtanguliza katika mambo yako  yote, na upendo huu ndio utasababisha mke awe na furaha wakati wote na haitakuwa ngumu kuonyesha utii wake kwa mumewe.
Kumbuka: Hata kama mume hajasimama kwenye nafasi yake, ni lazima wewe uonyeshe heshima, upendo na utii kwake bila kujali yeye anakutendea nini. Muombe Mungu akuwezeshe maana kibinadamu yaweza kuwa ngumu sana.
Mungu akubariki sana.

No comments: