MUNGU WETU NI MOTO ULAO WAEBRANIA 12:29.

Tuesday, January 23, 2018

KUFUNGA MALANGO YA KUZIMU NA KUHARIBU JESHI LA KUZIMU



Na Bishop Dankton Rudovick Rweikila

21st January 2018  

Jana tulianza somo hili na tuliangalia namna kuzimu inavyoweza kufungua kinywa chake na kuachilia tamaa. Na tuliona namna ambavyo kuzimu ikiachilia tamaa jinsi inavyokuwa na kwa faida ya wale ambao hawakuwepo tiliangalia kwa undani kidogo na ningekushauri upate mafundisho ya jana kwa kupitia namber zetu hapo chini ili uende vizuri na mfululizo wa masomo haya.

Tuliangalia

Isaya 5:13-14 13 Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na watu wao wenye cheo wana njaa, na wengi wao waona kiu sana.
14 Kwa hiyo kuzimu kumeongeza tamaa yake, kumefunua kinywa chake bila kiasi; na utukufu wao, na wingi wao, na ghasia yao, naye pia afurahiye miongoni mwao, hushuka na kuingia humo. 

Kwa hiyo kuzimu ikifungua kinywa chake ndipo utaona watu wanatamaa ya kupata utajiri kwa njia ya kutoa kafara, kufanya mambo mengi yasiyokuwa mapenzi ya Mungu. Kwa hiyo tuliangalia namna ambavyo kuzimu ikiongeza tamaa yake inavyokuwa.

Lakini tuliangalia namna ambavyo tunamamlaka juu ya kuzimu na tukaona pia kuwa kuzimu ina malango yake. Na Yesu kwa kupitia Petro alitupa ujumbe huu sisi kama kanisa la leo ili tujue kwamba tunayo mamlaka juu ya kuzimu.

Mathayo 16:18 18 Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. 19 Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni. 

Kwa hiyo kama kuzimu inaachilia tamaa kutesa maisha yako leo tunaifunga kwa jina la Yesu. Tuliona kuzimu ipo na leo tunaitembelea kuzimu kwa njia nyingine na kuangalia inatendaje kazi. Tayari kuzimu ipo na ina kinywa inayo malango na tamaa zake. Kuna watu ambao wanajenga nyumba zao na wanaomba lakini wanashangaa bado wanavamiwa, JUA KWAMBA KUNA LANGO LA KUZIMU MAHALI HAPO. Jana wakati ninafungua watu niliona kitu kimoja cha ajabu sana kuna mama mmoja ambaye kwenye TV yake ndipo yalipo malango ya kuzimu na kwenye makocho yake.

NAMNA KUZIMU INAVYOTENDAKAZI

Ufunuo 16:13-14 13 Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo.
14 Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi. 

Roho kutoka kuzimu inaweza kuvaa sura ya wanyama mbali mbali au wanadamu ilimradi itende kazi duniani. Roho kutoka kuzimu haiwezi kufanya kazi bila kuvaa umbo la Duniani. Hiyo ndiyo mifumo Mungu aliiweka tangu kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu huu, kwa hiyo kisicho na mwili au umbo la vitu ambavyo viko duniani haviwezi kuishi Duniani.

Kama kuzimu inatenda kazi Duniani kuna wajumbe wake kutoka kuzimu ambao wanatenda kazi Duniani. Kama ambavyo unaona mtu ambaye yuko duniani ila ana Roho ya Bwana kutoka mbinguni. Kwa hiyo ni mwanadamu wa kawaida lakini anao uweza wa kimbingu ambao siyo wa kawaida. Yesu aliwaambia wanafunzi wake wasiondoke humo mjini mapaka wamevikwa uweza kutoka juu yaani Roho Mtakatifu. Kuzimu vile vile ina watu wake ambao wamejaa roho za ubaya kutoka kuzimu, wanaishi kama wanadamu, kula, kunywa na kuvaa lakini ni mawakala wa kuzimu.

ROHO ZA KUZIMU ZINAZOVAA MAUMBO

Yohana aliona Roho tatu kama vyura lakini si vyura bali ni roho zilizotoka kwenye kinywa cha joka. Joka aliachilia Roho na ikamvaa mwanadamu ambaye anaitwa nabii wa uongo. Kwa hiyo hautaona joka bali utaona mwanadamu lakini ndani yake ana Roho ya joka. Nabii wa uongo kwa tafsiri rahisi ni mwanadamu ambaye anamtumikia shetani.

Maombi

Kwa jina la Yesu kwa damu ya Yesu tunawateka manabii wa uongo wote kutoka kuzimu kwa jina la Yesu. Tunawateka Wachungaji wa uongo, mitume na waalimu wa uongo leo tunawateka nyara kwa jina la Yesu. Tunaziteka madhabahu zao nyara kwa jina la Yesu leo tunapasua madhabahu zao kwa Damu ya Yesu. Leo tunashambulia vinywa vyao vya vinavyotoa maneno ya uongo kwa jina la Yesu. Tunapindua pindua mahali pao leo kwa jina la Yesu. Tunafuta kila utabiri wao wa uongo kwa damu ya Yesu kila maneno ya uongo wanayoyatoa leo tunayapatilisha kwa jina la Yesu.


Biblia inaongelea kuhusu nabii wa uongo, na shetani akafunga watu fahamu zao ili waone kuwa nabii wa uongo ni wale wanaotokea sasa. Kwa hiyo watu wanadhani wale waliooanza kazi ya kuhubiri kitambo hawawezi kuwa manabii wa uongo sikiliza nikuambie nabii wa uongo haijalishi ana kanisa la ukubwa kiasi gani bado ni nabii wa uongo tu. Shetani hawezi kujipinga siku zote. Kwa hiyo nabii wa uongo anachokifanya ni kukujaza Imani ya uongo, ukishapewa chumvi, sindano, ndimu na vitu kama hivyo hauna tofauti na wanaologa. Imani yetu haiko kwenye vitu bali katika Kristo na Kristo ni NENO LAKE. Kwa hiyo usijaribu kutafuta mbadala wa Yesu, ndiyo maana nilisema watu wametekwa na kunyanganywa maarifa yakutambua kweli ya neno la Mungu.

Biblia inasema ufalme wa Mungu unatekwa na watu wenye nguvu siyo mtu kwa hiyo usikubali kubweteka ili uombewe tu lazima uombe sana. Usikubali kusomewa tu neno soma neno, usikubali kuambiwa tu ya Rohoni nilazima uyatafute ya rohoni kwa jina la Yesu. Biblia inasema nyakati za mwisho Bwana atamimina Roho yake kwa kila mwenye mwili.

Pazia la hekalu limekwishapasuka na kila mtu anaweza kusogea patakatifu pa patakatifu kwa Damu ya Yesu. Mtafute Mungu acha uvivu. Mtu aliyebeba Roho ya Shetani hauwezi kupigana nae pasipo wewe kubeba Roho ya Mungu. Kwa hiyo mwanadamu wa kawaida hawezi kupigana na roho hizo wala kuzijua pasipo kupokea Roho wa Mungu.

Ukishapokea Roho wa Mungu unakuwa na mamlaka ya jina lipitalo majina yote. Lile neno unalolitoa ndani yako linasukumwa na nguvu ya Roho Mtakatifu iliyopo ndani mwako.

“Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara”

Nilisema mara kadhaa kwamba usiangalie sana miujiza kwasababu unaweza kupotea. Wengi sana wamepotea kwa nyakati hizi na kudhani kwamba ishara ndiyo nguvu ya Mungu. Kama hapa ningekuwa naombea watu na wanaruka sarakasi watu wasingechoka hata kwa masaa matano lakini nikiachilia maarifa na kusema uombe watu wanachoka wanatamani kuona miujiza tu na ishara. Natamani ujue kuomba na kusoma neno badala ya kutamani ishara na maajabu unayoyaona, kumbuka ninapomfungua mtu anafunguka yeye na wewe unayetizama haupati kitu chochote zaidi ya kutizama mwingine akipokea. Tamani kuomba sana na kusoma neno sana ili uweze kumjua adui yako mwenyewe.

Ni wengi sana wanashuhudia lakini ukifuatilia ushuhuda wao siyo katika kweli yote, sasa ushuhuda wa namna hiyo mimi sikubaliani nao kwasababu njia iliyompeleka huyo mtu kwenye ushuhuda utakuta siyo njia halali, kwa hiyo tunafurahia kumbe ni ushuhuda wakutoka kuzimu.

Inawezekana ulikuwa unapigana kwa kuchukia wanadamu lakini leo nataka kukuonyesha yule ambaye tunapigana naye kila siku siyo mwanadamu.

Ufunuo wa Yohana 18:2 Akalia kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza; 


Roho chafu inaweza kutembea bila kuiona kwa macho ya nyama. Lakini nguvu iliyondani yako inaweza kufichua yale yasiyoonekana kwa macho ya nyama.

Unayo mamlaka ya kutupa Roho chafu aliyokutupia shetani na ukaitupa nje kwa jina la Yesu.
Yohana 12:31-32 31 Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje. 32 Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu. 

Shetani ana makao ndani yako yeye ni mwizi na amevamia tu, kwa hiyo kila nguvu iliyondani yako ambayo ni ya kuzimu Yesu ataiondoa na kuitupa nje. Mkuu wa ulimwengu huu ni shetani na ndiye tunamtupa nje kwa jina la Yesu.


Shika moyo wako tuombe

Ninakamata kila Roho chafu za kuzimu ndani yangu kwa jina la Yesu kwa Damu ya Yesu.
Ewe chuki ewe kiburi nakutupa nje kwa jina la Yesu. Ewe Roho chafu ndani yangu ninakutupa nje kwa jina la Yesu. Ninalipua leo Roho ya chuki iliyondani yangu kwa jina la Yesu. Ninapiga leo maskani ya Roho zote chafu kwa jina la Yesu. Roho ya uasi uliyo ndani yangu ninakungoa na kukutupa nje kwa jina la Yesu. Ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, wewe ni Roho ninakutupa nje kwa jina la Yesu.  

Achia mwili wangu kwa jina la Yesu imeandikwa mwili wangu ni hekalu la Roho Mtakatifu kwa jina la Yesu. Achia hekalu la Bwana kwa jina la Yesu.


Tuonane kwenye maombi siku ya kesho saa kumi kamili


Mungu akubariki sana

No comments: