MUNGU WETU NI MOTO ULAO WAEBRANIA 12:29.

Friday, November 04, 2016

JE...... NI KIPI KITAKACHOANZA KATI YA DHIKI KUU NA UFUFUO?



Mathayo 24:
9 Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu.

10 Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana.

13 Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.

BIBLIA INASEMA
Watakatifu watachukiwa kwa ajili ya jina la Yesu
Swali ni watu gani wanaochukiwa kwa ajili ya jina la Yesu kama sio wale wanaoyafata mapenzi ya Mungu?

HII inaonesha kuwa watakatifu watakuwa katika dhiki kuu
  Katika dhiki hiyo mwenye kuvumilia ndiye atakayeokoka.. Bila shaka wenye kuvumilia ni wale walio na Yesu maana wataipitia dhiki kuu.

TENA BIBLIA INASEMA KATIKA DHIKI HIYO SIKU ZISINGELIFUPIZWA ASINGEOKOKA MTU YEYOTE MAANA WATAKATIFU WATATESWA KATIKA DHIKI HIYO.

Mathayo 24: 21 Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe.
22 Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo.

JE BAADA YA DHIKI KUU NI NINI KITAFATA?

Mathayo 24: 29 Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika;
30 ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi.

  Biblia inasema itaanza dhiki na wale watakao vumilia hadi mwisho katika dhiki kuu ile pasipo kumkana Yesu wataokoka Yesu akija kuwachukua.

JE WATAOSHINDA KATIKA DHIKI KUU NA KWENDA MBINGUNI, JE HUKO MBINGUNI WATASEMAJE JUU YAO?
Ufunuo 7:13 Akajibu mmoja wa wale wazee akiniambia, Je! Watu hawa waliovikwa mavazi meupe ni akina nani? Na wametoka wapi?
14 Nikamwambia, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo.
  Shetani atatafta kila njia ya kutaka watu wapigwe chapa ya mnyama
Lakini habari njema ni kwamba wale watakao kuwa wamempokea Yesu wa kweli watashinda.









Mafundisho Pale Mlima Wa Mizeituni
Hebu tuanze kwa kutazama sura ya 24 ya Injili ya Mathayo, sehemu ya Maandiko ambayo ni ya msingi sana kwa habari ya matukio ya nyakati za mwisho na kurudi kwa Yesu. Pamoja na sura ya 25, sehemu hiyo huitwa Mafundisho Pale Mlima Wa Mizeituni, kwa sababu sura hizo mbili ni taarifa ya mahubiri ambayo Yesu alitoa kwa baadhi ya wanafunzi Wake wa karibu sana[3] hapo mlimani. Tunaposoma mafundisho hayo, tutajifunza kuhusu matukio mengi ya nyakati za mwisho, nasi tutaona uwezekano wa wanafunzi wa Yesu kufikiri muda wa Unyakuo ni upi, waliposikia mafundisho yenyewe.

Yesu akaenda zake, akatoka hekaluni. Wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya hekalu. Naye akajibu akawaambia, ‘Hamyaoni haya yote? Amin nawaambieni, halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa.’Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha wakisema, ‘Tuambie! Mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia?’ (Mathayo 24:1-3).
Wanafunzi wa Yesu walitaka kujua habari za wakati ujao. Sana sana walitaka kujua majengo ya hekalu yangebomolewa lini (kama Yesu alivyokuwa ametabiri) na ishara gani ingeonyesha wakati wa kurudi Kwake na mwisho wa wakati.
Ukilitazama hivyo, tunajua kwamba majengo ya hekalu yalibomolewa kabisa mwaka wa 70 B.K. na jemadari Tito, akiongoza majeshi ya Kirumi. Pia tunajua kwamba Yesu bado hajarudi kujichukulia kanisa Lake, kwa hiyo, hayo matukio mawili hayafuatani, wala hayatokei wakati mmoja.
Yesu Ajibu Maswali Yao
Inaonekana kwamba Mathayo hakuandika jibu la Yesu ka swali la kwanza, kuhusu kuharibiwa kwa majengo ya hekalu baadaye. Ila, Luka alifanya hivyo katika Injili yake (ona Luka 21:12-24). Katika Injili ya Mathayo, Yesu alianza moja kwa moja kuzungumza kuhusu ishara ambazo zingetangulia kurudi Kwake mwisho wa wakati.
Yesu akajibu akawaambia, ‘Angalieni mtu asiwadanganye [ninyi]. Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi. Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni [ninyi] msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifal na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa na matetemeko ya nchi mahali mahali. Hayo yote ndiyo mwanzo wa utungu.’ (Mathayo 24:4-8. Maneno mepesi kukazia).
Kutokana na jinsi mahubiri hayo yalivyoanza, ni dhahiri kwamba Yesu aliamini kwamba hao wanafunzi Wake wa karne ya kwanza wangekuwa hai wakati ishara hizo zinazotangulia kurudi Kwake zinapotendeka. Ona anasema nao moja kwa moja, kibinafsi. Katika sura hii ya 24, Yesu anasema na wanafunzi Wkae moja kw amoja zaidi ya mara ishirini. Basi, wasikilizaji Wake wote wangeamini kwamba wataishi na kuona hayo yote ambayo Yesu ametabiri.
Lakini ni kweli kwamba wanafunzi wote waliomsikiliza Yesu siku hiyo wamekufa siku nyingi sana. Ila, tusidhani kwamba Yesu alikuwa anawadanganya. Yeye Mwenyewe hakujua wakati atakaporudi (ona Mathayo 24:36). Kweli ilikuwa inawezekana kwa wale waliosikiliza mafundisho Yake pale Mlima wa Mizeituni kuwa hai wakati wa kurudi Kwake.
Kilichokuwa cha msingi kabisa kwa Yesu ni kwamba wanafunzi Wake wasidanganywe na makristo wa uongo, kama itakavyokuwa katika siku za mwisho. Tunajua kwamba Mpinga Kristo mwenyewe atakuwa kristo wa uongo, na atadanganya dunia kwa sehemu kubwa. Watuw atamhesabu kuwa mwokozi mzuri sana.
Yesu alisema zitakuwepo vita, njaa na matetemeko, lakini pia alionyesha kwamba hayo matukio si ishara za kurudi Kwake bali ni “mwanzo wa utungu” tu. Ni salama kusema kwamba matukio hayo yamekuwepo kwa miaka zaidi ya elfu mbili iliyopita. Ila, anachosema Yesu baada ya hapo ni kitu ambacho hakijatokea.
Dhiki Inaaza Katika Dunia Nzima
Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukuwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana na kuchukiana. Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja (Mathayo 24:9-14. Maneno mepesi kukazia).
Hapa tena – kama ungewauliza wale waliomsikiliza Yesu siku hiyo swali hili: “Je, mnatazamia kuwa hai ili kuona kutimia kwa mambo hayo?” bila shaka wangejibu ndiyo kwa uhakika sana, maana Yesu alisema nao moja kwa moja.
Kama tulivyosoma – mara tu baada ya “utungu” kuna tukio ambalo kweli halijatokea, la wakati wa Wakristo duniani kote kuteswa. Tutachukiwa na “mataifa yote”. Yesu alikuwa anazungumza juu ya wakati fulani ambapo hayo yangetokea – si kipindi cha jumla cha miaka mia nyingi, maana alisema hivi baada ya hayo, “Ndipo wengi watakapojikwaa,nao watasalitiana na kuchukiana.”
Bila shaka anachosema hapo kinahusu kurudi nyuma kwa waamini Wakristo ambao baada ya hapo watawachukia waamini wengine, maana wasioamini hawawezi “kuanguka,” tena, wanachukiana tayari. Basi, mateso ya dunia nzima yatakapoanza, kutakuwa na kurudi nyuma kwa watu wengi wanaodai kwamba ni wafuasi wa Kristo. Kama ni wakweli au ni waamini bandia – yaani kondoo au mbuzi – wengi sana wataanguka, nao watafichua majina ya waamini wengine kwa watesaji, wakiwachukia wale waliodai kuwapenda. Matokeo ni kwamba kanisa duniani kote litasafishwa.
Halafu tena kutakuwa na ongezeko la manabii wa uongo, na mmoja anatajwa sana katika kitabu cha Ufunuo kuwa mwenzake mpinga Kristo (ona Ufunuo 13:11-18; 19:20; 20:10). Maasi yataongezeka na kufikia mahali pa kumaliza kabisa upendo kidogo utakaokuwa umesalia mioyoni mwa watu, na wenye dhambi watakuwa wabaya kukithiri.
Wafia Dini Na Watakaosalia
Ingawa Yesu alitabiri kwamba waamini watapoteza maisha yao (ktk 24:9), si wote, maana aliahidi kwamba wale watakaovumilia mpaka mwisho wataokolewa (ona 24:13). Yaani, kama hawataruhusu wadanganywe na wale makristo wa uongo au manabii wa uongo, na kama watashinda jaribu la kuacha imani yao na kuanguka, wao wataokolewa na Kristo wakati anaporudi ili kuwakusanya mawinguni. Huu wakati wa dhiki baadaye pamoja na ukombozi wake ulifunuliwa kidogo kwa nabii Danieli pia. Yeye aliambiwa hivi
Na kutakuwa wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile. Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele (Danieli 12:1, 2).
Wokovu bado utatolewa kwa neema hata katika siku hizo, maana Yesu aliahidi kwamba Injili itahubiriwa kwa mataifa yote, kutoa nafasi moja ya mwisho ya kutubu, ndipo mwisho utakapokuja.[4] Tunasoma kitu katika Kitabu cha Ufunuo ambacho kinaweza kuwa kutimizwa kwa ahadi ya Yesu.
Kisha nikaona malaika mwingine akiruka katikati ya mbingu, mwenye Injli ya milele, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa. Akasema kwa sauti kuu, ‘Mcheni Mungu na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji’. (Ufunuo 14:6, 7. Maneno mepesi kukazia).
Kuna wanaodhani kwamba sababu ya malaika kuhubiri Injili wakati huo ni kwamba, kufikia hapo katika kipindi cha dhiki ya miaka saba, Unyakuo utakuwa umetokea na waamini wote watakuwa wameondoka. Lakini, hayo ni mawazo tu.
Mpinga Kristo
Nabii Danieli alifunua kwamba mpingakristo atakuwa na nafasi katika hekalu la Yerusalemu litakalojengwa upya, katikati ya ile miaka saba ya dhiki, na kujitangaza kwamba ni Mungu (ona Danieli 9:27 – tutajifunza baadaye). Tukio hili ndilo Yesu anazungumzia alipoendelea kufundisha pale Mlima wa Mizeituni, kama ifuatavyo:
Basi, hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani; naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake; wala aliye shambani asirudi nyuma kuchukua nguo yake. Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo! Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato. Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe.[5] Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu yeyote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo (Mathayo 24:15-22).
Hayo ni maelezo yaliyo dhahiri zaidi kuhusu dhiki ambayo Yesu alizungumzia mapema (ktk 24:9). Wakati mpingakristo atakapotangaza kwamba yeye ni Mungu kutoka hekalu la Yerusalemu, mateso yasiyofikirika yatatokea dhidi ya wanaomwamini Yesu. Kwa kujitangaza kwamba yeye ni Mungu, mpingakristo atatazamia kilamtu kutambua uungu wake. Basi, wafuasi wote wa kweli wa Kristo watakuwa maadui wa taifa, watu wa kusakwa na kuuawa. Ndiyo sababu Yesu aliwaambia waamini wa Uyahudi wakimbilie milimani bila kukawia, wakiomba kwamba kutoroka kwao kusizuiwe na sababu yoyote ile.
Wazo langu ni kwamba ingekuwa vizuri kwa waamini wote duniani kukimbilia maeneo yaliyofichika wakati huo, maana tukio hilo litatangazwa duniani kote kwa njia ya televisheni. Maandiko yanatuambia kwamba dunia nzima itadanganywa na mpingakristo na kudhani yeye ndiye Kristo wao, nao watampa mamlaka na heshima zote. Atakapojitangaza kwamba ni Mungu, watamwamini na kumwabudu. Atakaponena makufuru dhidi ya Mungu wa kweli – Mungu wa Wakristo – atashawishi dunia yote iliyodanganyika ili kuwachukia wale wanaokataa kumwabudu (ona Ufunuo 13:1-8).
Yesu aliahidi ukombozi kwa ajili ya watu Wake mwenyewe kwa “kukatisha” hizo siku za dhiki, vinginevyo, “asingeokoka mtu yeyote” (24:22). Huko “kukatizwa” siku hizo Naye “kwa ajili ya wateule” bila shaka ni kitu kinachohusu Yeye kuwakomboa wakati atakapoonekana na kuwakusanya mawinguni. Yesu hata hivyo hatuambii hapa kwamba ukombozi huo utatokea muda gani baada ya mpingakristo kujitangazia uungu.
Vyovyote vile – tunarudia kusema hapa tena kwamba Yesu aliwaacha wasikilizaji Wake siku hiyo wakiwa wanajua kwamba wangeishi na kumwona mpingakristo akitangaza uungu wake, na kupigana vita na Wakristo. Hili linapingana kabisa na wazo la wale wanaosemakwamba waamini watanyakuliwa kabla ya tukio hilo. Kama ungemwuliza Petro, Yakobo au hata Yohana kwamba Yesu angerudi kuwaokoa kabla ya tamko la mpingakristo kwamba ni Mungu, wangekujibu, “Si hivyo”.
Vita Dhidi Ya Watakatifu
Katika sehemu zingine, Maandiko yanatabiri juu ya mateso ya mpingakristo kwa waamini. Kwa mfano: Yohana alifunuliwa, naye akaandika hivi katika kitabu cha Ufunuo:
Naye [mpingakristo] akapewa kinywa cha kunena maneno makuu, ya makufuru. Akapewa uwezo wa kufanya kazi yake miezi arobaini na miwili. Akafunua kinywa chake amtukane Mungu, na kulitukana jina lake, na maskani yake, nao wakaao mbinguni. Tena akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda, akapewa uwezo juu ya kila kabila na jamaa na lugha na taifa (Ufunuo 13:5-7. Maneno mepesi kukazia).
Ona hapo kwamba mpingakristo atapewa “uwezo wa kufanya kazi yake” kwa miezi arobaini na mbili, au, miaka mitatu na nusu kamili. Huu ndiyo wakati unaoitwa nusu ya wakati wa kipindi cha Dhiki ya miaka saba. Ni sawa kabisa kufikiri kwamba ni ile miezi arobaini na mbili ya mwisho ya Dhiki, ndipo mpingakristo atakapopewa “uwezo wa kufanya kazi yake,” kwa sababu mamlaka yake yataondolewa kabisa wakati Kristo atakaporudi kufanya vita naye na majeshi yake wakati wa kumalizika kwa Dhiki.
Ni dhahiri kwamba “uwezo wak ufanya kzi yake” kwa miezi arobaini na mbili maan ayake ni mamlaka maalum, maana mpingakristo atapewa mamlaka kiasi fulani na Mungu katika wakati wake wa kumiliki. Haya “mamlaka maalum ya kufanya kazi” yanaweza kuwa ni muda atakaopewa wa kuwashinda watakatifu, maana, tunasoma hivi katika kitabu cha Danieli:
Nikatazama, na pembe iyo hiyo [mpingakristo] ilifanya vita na watakatifu, ikawashinda; hata akaja huyo mzee wa siku [Mungu], nao watakatifu wake Aliye Juu wakapewa hukumu; na majira yakawadia watakatifu waumiliki ufalme. … Naye [mpingakristo] atanena maneno kinyume chake Aliye Juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye Juu; naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati (Danieli 7:21, 22; 25. Maneno mepesi kukazia).
Danieli alitabiri kwamba watakatifu wangetiwa mikononi mwa mpingakristo kwa “wakati, nyakati, na nusu wakati.” Maneno hayo yaeleweke kwamba ni miaka mitatu na nusu, kama utafananisha na Ufunuo 12:6 na 14. Tunaambiwa katika Ufunuo 12:6 kwamba mwanamke fulani ambaye ni mfano, atapewa mahali pa kujificha nyikani ili “atunzwe na kulishwa” huko kwa muda wa siku 1,260, ambazo ni sawa na miaka mitatu na nusu kwa mwaka wenye siku 360. Kisha, mistari nane baadaye, anatajwa tena, na wakati huo inasemekana atapewa mahali nyikani ili “atunzwe na kulishwa” kwa “wakati, nyakati, na nusu ya wakati.” Basi, “wakati, nyakati, na nusu ya wakati” ni sawa na zile siku 1,260, au miaka mitatu na nusu.
Kumbe katika mantiki hii, neno “wakati” maana yake mwaka, na “nyakati” maana yake miaka miwili, na “nusu ya wakati” maana yake nusu mwaka. Lugha hii ya ajabu inayopatikana katika Ufunuo 12:14 bila shaka ina maana kama katika Danieli 7:21. Basi, sasa tunajua kamba watakatifu watatiwa mikononi mwa mpingakristo kwa miaka mitatu na nusu, ambao ndiyo muwa ule ule tunaoambiwa katika Ufunuo 13:5 kwamba mpingakristo atapewa “uwezo wa kufanya kazi yake.”
Mimi nadhani vipindi hivyo viwili vya miezi arobaini na mbili vinafanana. Kama vitaanza wakati wa mpingakristo kujitangaza kwamba ni Mungu katikati ya ile Dhiki ya miaka saba, basi ni kwamba watakatifu watatiwa mikononi mwake kwa miaka mitatu na nusu inayofuata, na Yesu atawakomboa atakapotokea mawinguni na kuwakusanya waende Naye wakati huo, au karibu na mwisho wa hiyo Dhiki. Lakini, kama hiyo miezi arobaini na mbili inaanza wakati mwingine katika kipindi cha Dhiki ya miaka saba, basi inatubidi tukubali kwamba Unyakuo utatokea wakati fulani kabla ya mwisho wa Dhiki ya miaka saba.
Tatizo la hoja hiyo ya mwisho ni kwamba inabidi watakatifu watiwe mikononi mwa mpingakristo kabla ya kuingia hatarini na kuhitaji kukimbilia milimani wakati anapojitangaza kuwa Mungu. Hilo ni gumu.
Tatizo la hoja ile ya kwanza ni kwamba watakatifu watakuwepo duniani bado wakati Mungu atakapokuwa anamimina hukumu duniani, tunazosoma katika kitabu cha Ufunuo. Tutatazama ugumu huo baadaye. Tuendelee na Mafundisho ya Mlima wa Mizeituni.
Masiya Wa Uongo
Ndipo Yesu akafafanua zaidi kwa wanafunzi Wake umuhimu wa kutodanganywa na habari kuhusu maKristo wa uongo.
Wakati huo mtu akiwaambia, ‘Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu, wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele. Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa popote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai (Mathayo 24:23-28).
Ona tena hapa jinsi Yesu anavyosema na wanafunzi moja kwa moja. Wasikilizaji Wake pale Mlima wa Mizeituni wangetazamia kuishi mpaka waone kutokea kwa makristo wa uongo na manabii wa uongo ambao wangetenda miujiza mikubwa. Na bila shaka wangetazamia kumwona Yesu akirudi mawinguni kama umeme.
Hatari ya kurudi nyuma wakati huo itakuwa kubwa sana, maana mateso dhidi ya waamini yatakuwa makali mno na makristo wa uongo na manabii wa uongo watashawishi watu sana kutokana na miujiza yao. Hii ndiyo sababu Yesu anarudia tena na tena kuwaonya wanafunzi Wake kuhusu yatakayotokea muda mfupi tu kabla ya kurudi Kwake. Hakutaka wao wapotoshwe kama itakavyokuwa kwa wengi. Waamini wa kweli na walio thabiti watamngoja Yesu arudi mawinguni kama umeme, ambapo wale wasiokuwa wafuasi Wake kweli watavutwa kwa makristo hao wa uongo kama tai wanavyovutiwa na mzoga nyikani.
Ishara Mawinguni
Yesu akaendelea hivi:
Lakini mara baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika, ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi. Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu (Mathayo 24:29-31).
Mifano au picha katika sehemu hii ya mafundisho ya Yesu pale Mlima wa Mizeituni bila shaka ingekuwa inafahamika na Wayahudi wa siku Zake, maana inatoka katika Isaya na Yoeli, na inazungumzia hukumu ya mwisho ya Mungu, mwisho wa dunia. Mara nyingi huitwa “siku ya Bwana”, wakati jua na mwzi vitatiwa giza (ona Isaya 13:10, 11; Yoeli 2:31). Ndipo wakazi wote wa dunia watakapomwona Yesu akirudi mawinguni katika utukufu Wake, nao wataomboleza. Kisha malaika wa Yesu “watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu,” kuonyesha kwamba waamini watanyakuliwa na kukusanywa ili kumlaki Yesu mawinguni, na hayo yote yatatokea baada ya mlio wa “baragumu”.
Hapa tena, kama ungemwuliza Petro, Yakobo au Yohana ikiwa Yesu angewarudia kabla au baada ya wakati wa mpingakristo na dhiki kuu, bila shaka wangesema, “Baada.”
Kurudi Kwake, Na Unyakuo
Hii sehemu ya Mafundisho ya pale Mlima wa Mizeituni inaeleweka sana, kulingana na tukio ambalo Paulo aliandika juu yake, ambalo bila shaka ni Unyakuo wa kanisa, ingawa waandishi wengi wa vitabu vya kufafanua Biblia wanasema linatokea kabla ya kipindi cha Dhiki kuanza. Hebu tazama andiko lifuatalo, tulilotazama mwanzoni mwa sura hii.
Lakini ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko,na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tuli hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. Basi, farijianeni kwa maneno hayo. Lakini ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku. Wakati wasemapo, Kuna amani n salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa (1Wathes. 4:13 – 5:3. Maneno mepesi kukazia).
Paulo aliandika juu ya Yesu kuja kutoka mbinguni kwa parapanda ya Mungu na kwamba waamini watanyakuliwa “mawinguni ili kumlaki Bwana hewani.” Ni sawa kabisa na yale Yesu aliyokuwa akieleza katika Mathayo 24:30, 31 – yanayotokea baada ya kutokea kwa mpingakristo na dhiki.
Tena, Paulo alipoendelea kuandika kuhusu kurudi kwa Kristo, anataja kwamba ingetokea lini – “majira na nyakati” – na kuwakumbusha wasomaji wake kwamba walikuwa wanafahamu vizuri sana kwmaba “siku ya Bwana ingekuja kama mwivi anavyokuja usiku.” Paulo aliamini kwamba kurudi kwa Kristo na Unyakuo wa waaminio ungetokea “siku ya Bwana,” siku ambapo hasira kali na maangamizi vingewapata wale waliokuwa wanatazamia “amani na salama.” Kristo anaporudi kulinyakua kanisa Lake, hasira Yake itashuka juu ya dunia.
Hili linakubaliana vizuri sana na kile ambacho Paulo aliandika katika barua kwa Wathesalonike baadaye, kuhusu kurudi kwa Kristo na hasira Yake.
Kwa kuwa ni haki mbele za Mungu kuwalipa mateso wale wawatesao ninyi; na kuwalipa ninyi mteswao raha pamoja na sisi; wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu,na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu; watakaoadhibiwa kwa maagamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake; yeye atakapokuja ili kutukuzwa katika watakaifu wake, na kustaajabiwa katika wote waliosadiki katika siku ile, (kwa sababu ushuhuda wetu ulisadikiwa kwenu). (2Wathes. 1:6-10. Maneno mepesi kukazia)
Paulo alisema kwamba wakati ambao Yesu angerudi kuwapa nafuu Wathesalonike waliokuwa wanateswa (ona 1Wathes. 1:4, 5), angetokea “pamoja na malaika wake katika mwali wa moto” ili kuwaadhibu wale waliokuwa wanawatesa wao, kutoa hukumu ya haki, inayostahili. Hii haifanani na kile kinachosemwa na wengi, kwamba Unyakuo utatokea kabla ya dhiki, na kanisa kunyakuliwa na Kristo kabla ya kile kipindi cha dhiki cha miaka saba kuanza. Hii pia huitwa kuja kwa siri kwa Yesu ili kunyakua kanisa Lake. Hapana kabisa! Maelezo haya yanafanana na kile ambacho Yesu alieleza katika Mathayo 24:30, 31 – kurudi Kwake karibu au mwishoni mwa kipindi cha dhiki kuu – anapowanyakua waaminio na kumimina hasira Yake juu ya wasoiamini.
Siku Ya Bwana
Baadaye, katika barua hiyo hiyo, Paulo aliandika hivi:
Basi ndugu, tunakusihini, kwa habari ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake, kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo (2Wathes. 2:1, 2).
Kwanza: Ona kwamba mada ya Paulo ni kurudi kwa Kristo na Unyakuo. Aliandika kuhusu “kukusanyika kwetu mbele zake,” akitumia maneno yale yale ambayo Yesu alitumia katika Mathayo 24:31, alipozungumza juu ya malaika ambao “wangekusanya” wateule Wake “kutoka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho ule.”
Pili: Ona kwamba Paulo anayaita matukio hayo kuwa ni “siku ya Bwana,” sawa na alivyofanya katika 1Wathesalonike 4:13 hadi 5:2. Hilo liko wazi kabisa.
Kisha anaendelea hivi:
Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yoyote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu; yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu (2Wathes. 2:3, 4. Maneno mepesi kukazia).
Wakristo Wathesalonike walikuwa wanadanganywa kwa namna fulani kwamba siku ya bwana – ambayo kulingana na Paulo lazima ianze kwa Unyakuo na kurudi kwa Kristo – ilikuwa imekwisha fika. Akatamka wazi wazi kwamba haiji mpaka baada ya ule ukengeufu (labda ndiyo kule kurudi nyuma ambako Yesu alizungumzia katika Mathayo 24:10) na baada ya mpingakristo kujitangaza kwamba ni Mungu kutoka hekalu la Yerusalemu. Basi, Paulo anawaambia waamini Wathesalonike wazi wazi kwamba wasitazamie kurudi kwa Kristo – au Unyakuo – wala siku ya Bwana, mpaka baada ya tamko la mpingakristo kwamba ni Mungu.[6]
Kisha, Paulo anaelezea kuhusu kurudi kwa Kristo na jinsi anavyomwangamiza kabisa mpingakristo.
Je, hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi naliwaambieni hayo? Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake. Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa. Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake; yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo; na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa (2Wathes. 2:5-10).
Paulo alitamka kwamba mpingakristo atakomeshwa “kwa ufunuo wa kuja Kwake” Kristo. Kama “ufunuo” Wake ni sawa na ule unaotajwa wakati wa Unyakuo – kiasi cha mistari tisa nyuma (ktk 2:1), basi mpingakristo atauawa wakati huo huo ambapo Kanisa litakusanywa ili kumlaki Bwana hewani. Hii inalingana na taarifa itolewayo katika Ufunuo sura ya 19 na 20. Hapo tunasoma juu ya kurudi kwa Kristo (ona Ufunuo 19:11-16), kuangamizwa kwa mpingakristo na majeshi yake (ona 19:17-21), kufungwa kwa Shetani (ona 20:1-3) na “ufufuo wa kwanza” (ona 20:4-6), ambapo waamini waliouawa katika kipindi cha Dhiki yamiaka saba watafufuliwa. Kama huu ndiyo ufufuo wa kwanza kweli kweli kwa maana ya jumla kwamba ni kwa ajili ya wenye haki, basi hakuna mashaka kwamba Unyakuo na kurudi kwa Kristo katika hasira Yake kunatokea wakati huo huo ambapo mpingakristo anaharibiwa, maana, Maandiko yanatuambia wazi kabisa kwamba wote waliokufa katika Kristo watafufuliwa wakati wa Unyakuo (ona 1Wathes. 4:15-17).[7]
Kuwa Tayari
Hebu turudi tena kwenye Mafundisho pale Mlima wa Mizeituni.
Basi kwa mtini jifunzeni mfano. Tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu. Nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni. Amin nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia.[8] Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe (Mathayo 24:32-35).
Yesu hakutaka wanafunzi Wake wanaswe bila kufahamu – na hilo ndilo jambo la msingi katika Mafundisho ya pale Mlima wa Mizeituni. Wangejua kwamba “yuko malangoni” baada ya kuona “mambo hayo yote” – dhiki duniani kote, kurudi nyuma kwa watu, kutokea kwa manabii na makristo wa uongo, tangazo la mpingakristo kwamba ni Mungu, na kutiwa giza jua na mwezi pamoja na kuanguka kwa nyota, wakati karibu na kurudi Kwake.
Ila, baada tu ya kuwaambia kuhusu ishara zitakazotangulia kuja Kwake kwa miaka michache, au miezi au siku, aliwaambia sasa wakati hasa wa kurudi Kwake ungebakia kuwa siri.
Walakini kwa habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake (Mathayo 24:36).
Mara nyingi andiko hili linatajwa kinyume cha mantiki yake! Kwa kawaida linatajwa ili kuunga mkono dhana kwamba hatuna habari Yesu atarudi lini, kwa sababu anaweza kurudi wakati wowote na kunyakua kanisa. Lakini katika mantiki yake, Yesu hakumaanisha hicho. Alikuwa ndiyo kamaliza kuhakikisha kwamba wanafunzi Wake wangekuwa tayari kwa ajili ya kurudi Kwake kwa kuwaambia ishara nyingi ambazo zingetokea muda mfupi tu kabla ya kurudi Kwake. Sasa anachowaambia ni kwamba, siku hasa na saa havitafunuliwa kwao. Tena, Yesu hasemi juu ya kuja Kwake mara ya kwanza kabla ya kipindi cha Dhiki ya miaka saba kuanza, wakati ambapo kanisa lingenyakuliwa, bali kuhusu kurudi Kwake wakati wa mwisho au karibia mwisho wa Dhiki. Hilo halina matatizo ukitazama mantiki vizuri.
Je, Kurudi Kwake Hakujulikani Kabisa?
Hoja ambayo mara nyingi hutumika dhidi ya Unyakuo kutokea karibu au wakati wa mwisho wa Dhiki ni kwamba kurudi kwa namna hiyo kusingekuwa kitu kisichojulikana kama Yesu alivyodaiwa kusema, kwa sababu kurudi kwa namna hiyo kungetazamiwa kwa matukio ya Dhiki. Lazima kuwe na Unyakuo kabla ya dhiki, la sivyo waamini wasingehitaji kuwa tayari na kukaa macho kama Maandiko yasemavyo wanapaswa kuwa, maana watajua ni miaka saba au zaidi kabla ya Yesu kurudi.
Ila, hoja hii inapingwa na ukweli kwamba lengo kuu la Mafundisho ya Yesu pale Mlima wa Mizeituni lilikuwa ni kuhakikisha kwamba wanafunzi Wake wawe tayari kwa ajili ya kurudi Kwake wakati au karibu na mwisho wa Dhiki, naye aliwafunulia ishara nyingi tu ambazo zingetangulia kuja Kwake. Mbona Mafundisho ya Mlimani yamejaa mashauri mengi sana kwamba watu wawe tayari na kuwa macho, ingawa Yesu alijua kwamba kurudi Kwake kuko mbele miaka mingi sana baada ya kusema maneno hayo? Bila shaka ni kwa sababu Yesu aliamini kwamba Wakristo wanahitaji kuwa tayari na kuwa macho hata ingawa kurudi Kwake bado kuko miaka mingi mbele. Mitume ambao katika barua zao waliwashauri waamini kuwa macho na kuwa tayari kwa ajili ya kurudi kwa Yesu walikuwa wanamwiga Yesu Mwenyewe.
Tena, wale wanaoamini kwamba Unyakuo kabla ya dhiki ndiyo wenye kuhalalisha mashauri yoyote ya kuwa tayari, wana tatizo lingine. Kulingana na mawazo yao, kurudi kwa Yesu mara ya kwanza hutangulia dhiki kwa miaka saba. Kwa hiyo, kurudi kwa Yesu mara ya kwanza kulingana na hoja zao hakuwezi kutokea wakati wowote – lazima itakuwa ni miaka saba kabla ya Dhiki kuanza. Basi, hakuna haja ya kutazamia kwamba Yesu atarudi mpaka matukio duniani yakamilike na kuwa tayari kuanza miaka saba ya Dhiki. Matukio hayo yanaweza kutazamiwa na kuhakikishwa kabisa.
Wengi wenye kuamini Unyakuo kabla ya dhiki – kama ni wakweli – watasema kwamba wanajua Yesu hatarudi leo wala kesho kwa sababu ya hali ya kisiasa duniani. Bado yapo matukio yaliyotabiriwa ambayo hayana budi kutimizwa kabla ya ile miaka saba ya Dhiki kuanza. Kwa mfano: Kama tutakavyoona katika kitabu cha Danieli, mpingakristo atafanya agano na Israeli kwa miaka saba, na huo utakuwa ndiyo mwanzo wa kipindi cha Dhiki. Hivyo basi, kama Unyakuo unatokea miaka saba kabla ya dhiki kuanza, lazima utokee wakati mpingakristo atakapofanya agano lake la miaka saba na Israeli. Basi, hakuna haja ya wale wanaoshikilia kwamba Unyakuo utafanyika kabla ya Dhiki kutazamia Yesu atarudi kabla ya kuona kitu katika siasa kinachofanya hayo yawezekane.
Zaidi ya hayo – kwa wale wanaoamini kwamba Unyakuo utatokea kabla ya dhiki, na kuamini kwamba Yesu atarudi mwishoni mwa Dhiki pia, maana yake ni kwamba siku kamili ya kurudi kwa Yesu mara ya pili inaweza kujulikana kimahesabu. Mara tu Unyakuo utokeapo, mtu yeyote angeweza kukadiria na kujua kile ambacho Yesu alisema ni Baba tu akijuacho. Unachofanya ni kuhesabu mbele miaka saba tu.
Tuseme tena hivi – Kutokana na yale ambayo Yesu alisema, Yeye hakutaka kurudi Kwake kuwe kitu cha kuwashtua watu. Ukweli ni kwamba alitaka kurudi Kwake kutazamiwe, na hivyo akataja matukio kadhaa ya Dhiki. Yesu hakutaka wanafunzi Wake wakutwe hawako tayari, kama ambavyo dunia itakutwa. Basi anaendelea kusema hivi katika Mafundisho Yake pale Mlima wa Mizeituni:
Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa kama vile siku zile ziliozkuwa kabla ya gharika watu walivyokuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa. Wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.[9] Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja (Mathayo 24:37-44).
Hapa tena, kitu ambacho Yesu anajali ni kwamba wanafunzi Wake wawe tayari kwa ajili ya kurudi Kwake. Hicho ndicho kilisababisha yote aliyosema kabla ya hapa na baada ya hapa, katika mafundisho Yake. Maonyo Yake mwengi kwamba wawe tayari na wakeshe si kwamba ni kwa kuwa kurudi Kwake kutakuwa kwa kushtukiza, bali ni ishara ya jinsi ambavyo itakuwa vigumu kwa sababu ya upinzani wa wakati wenyewe, kuendelea kuwa macho na kuwa tayari. Basi, wale wanaotarajia Unyakuo kabla ya Dhiki, wakati wowote, wanaodhani kwamba wako tayari kuliko Wakristo wengine, wanaweza wasiwe tayari kwa uhalisi kabisa, kwa kile kinachokuja. Kama hawatazamii dhiki yoyote na wajikute katikati ya mateso ya dunia nzima, wakati wa utawala wa mpingakristo, jaribu la kuanguka linaweza kuwazidi nguvu. Afadhali kuwa tayari kwa kile kinachofundishwa na Maandiko kwamba kitatokea.
Halafu tena – kama ungemwuliza Petro, Yakobo au Yohana kwamba walitazamia kumwona lini Yesu akirudi, wangekwambia kuhusu ishara hizo zote ambzo Yesu aliwaambia zingetokea, kabla ya kurudi Kwake. Wasingetazamia kumwona kabla ya kipindi cha dhiki, au kutokea kwa mpingakristo.
Mwivi Usiku
Ona kwamba hata mfano wa Yesu wa “mwivi usiku” uko katika mantiki ya Yeye kudhihirisha ishara nyingi ambazo zingewasaidia wanafunzi Wake wasinaswe ghafula kwa kurudi Kwake. Basi, mfano huo hauwezi kutumiwa kisahihi kuonyesha kwamba hakuna mtu anayeweza kuwa na wazo lolote kuhusu Yesu anarudi lini.
Paulo na Petro walitumia mfano wa Yesu wa “mwivi usiku” walipokuwa wanaandika kuhusu “siku ya Bwana” (ona 1Wathes. 5:2-4; 2Petro 3:10). Waliamini huo mfano ulikuwa na maana kwa habari ya Yesu kurudi kwa ghadhabu wakati wa au mwisho wa Dhiki ya miaka saba. Ila, Paulo aliwaambia hivi wasomaji wake: “Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi” (1Wathes. 5:4). Yeye alitafsiri kwa usahihi mfano wa Yesu, akitambua kwamba wale walio macho na makini kuona zile ishara, na wenye kumfuata Yesu kwa utiifu, hawakuwa gizani mpaka kuja kwa Kristo kuwapate kwa ghafula. Kwa watu namna hiyo, Yesu asingekuja kama mwivi usiku. Ni wale walio gizani tu ndiyo wangeshtushwa – na ndivyo Yesu alivyofundisha. (Ona vile vile matumizi ya Yesu ya maneno “mwivi usiku” katika Ufunuo 3:3 na 16:15. Hapo anatumia maneno hayo kusema juu ya kuja Kwake kwenye vita ya Har-magedoni.)

Kuanzia hapa na kuendelea katika Mafundisho Yake ya pale Mlima wa Mizeituni, Yesu alirudia kuwaonya wanafunzi Wake kuwa tayari kwa ajili ya kurudi Kwake. Hapo hapo akawaambia pia jinsi ya kuwa tayari, aliposema mifano kuhusu mtumwa asiyekuwa mwaminifu, kuhusu wanawali kumi, na kuhusu talanta, na baadaye akatabiri hukumu ya kondoo na mbuzi (yote inafaa kusomwa). Katika hiyo mifano yote, aliwaonya kwamba jehanamu ilikuwa inawasubiri wale wote wasiokuwa tayari kwa ajili ya kurudi Kwake (ona Mathayo 24:50, 51; 25:30, 41-46). Njia ya kuwa tayari ni kupatikana ukifanya mapenzi ya Mungu, wakati Yesu atakaporudi.[10]

No comments: