MUNGU WETU NI MOTO ULAO WAEBRANIA 12:29.

Thursday, January 11, 2018

KUTOKA UTUMWANI

Mkesha wa Alhamisi

Na Bishop Dankton Rudovick Rweikila
11th January 2018


Matendo ya mitume 23:10-12 10 Ugomvi mkubwa ulipotokea, yule jemadari akachelea Paulo asije akararuliwa nao, akaamuru askari washuke na kumwondoa kwa nguvu mikononi mwao, na kumleta ndani ya ngome. 11 Usiku ule Bwana akasimama karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako. 12 Kulipopambauka, Wayahudi wakafanya mapatano, wakajifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala hawatakunywa hata wamwue Paulo. 

Wakafanya mapatano…..

Sema kwa jina la Yesu kwa Damu ya Yesu ninavunja kila mapatano ya kichawi kwa jina la Yesu kwa Damu ya Yesu.

Wayahudi walijifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala hawatakunywa hata wamwue Paulo. Hiki kinaitwa kiapo cha kudhamiria na ndivyo wachawi wanafanya kudhamiria mpaka jambo litokee. Na ndiyo maana mkesha uliopita nilisema udhamirie kwamba katika maombi haya ya siku ishirini na moja jambo moja litokee. Kama wachawi wameapa na kudhamiria usiku na mchana kwamba awatakula mpaka biashara yako, watoto, ndoa, karama, elimu na mengine mengi yaharibike. Usiogope kama wamedhamiria na wewe umedhamiria na Mungu wako, uwe na moyo mkuu. Usiku ule ule Mjomba wake Paulo akasikia habari hizi na akampasha Paulo na wakamtorosha Paulo. Yapo mazuri ninayaona mbele yako japo wanashindana na wewe lakini hawatashinda. Kumbe ukipatana na wachawi nao wanapatana kwa kiapo kwa hawatakula wala kunywa mapaka Roho ya Paulo imetoka. Kuna watu wamekula kiapo kwamba hawatakula wala kunywa mpaka wewe umekwisha. Mungu anasema huwe na moyo mkuu bado una shughuli ya kufanya. Wamepanga ufe lakini Mungu anasema bado una kazi ya kufanya.

Viapo vya namna hii vinatenguliwa na watu wanaojitambua, kwasababu ni kiapo cha watu waliodhamiria na kinahitaji watu waliodhamiria ili kutengua. Ninajua kuna watu hapa wamenyooshewa vidole kwamba tutaona kama utakuwa na hiki au kile leo na sisi tunawanyooshea kidole cha Mungu aliye hai. Usiogope! Waliopanga kukuogopesha leo tunawaogopesha kwa jina la Yesu, Hata kama wanakishindo usiogope. Unakumbuka lile jeshi la washami ambalo lilikuwa na kishindo lakini lilikimbizwa na wakoma wanne. Kipindi kile kulikuwa na njaa sana kule Samaria na ikafikia mpaka watu walikula mavi ya njia kwa manunuzi ya vipande vitano vya fedha. 2Wafalme 6:25-33

Leo ninahitaji tuwe majasiri kama WALE WAKOMA, walisema tutabaki hapa mpaka lini kama tukibaki tutakufa wqkasonga mbele. USIOGOPE WAKO WATU WATAKUKIMBIA LEO. Wale waliokucheka watakukimbia, Boss wako atakukimbia, walikudharahu watakukimbia embu simama kama wakoma na kula kiapo ili uweze kusonga mbele. Wakoma hawakuwa na jeshi wala silaha lakini walipokula kiapo kwenye nafsi zao waliamua kuondoka. Kama wakoma wasingeliondoka jeshi la washami lisingesogea kokote. Usimuogope ADUI YAKO muendee na utashangaa namna atakavyokukimbia. 2 Wafalme 7:4-8

Maandiko yanasema wana wa Israeli wakati wanatoka misri Bwana aliachilia mapigo kumi, Mungu aliwapiga pigo la kumi na Farao akawaachia na mimi leo ninakutangazia utatoka na ninaona kitabu chako cha kutoka kimeandikwa, utatoka kwenye umaskini, shida, kudharaulika. Ninapoongelea kutoka sina maana ya kitabu cha kutoka kwenye Biblia ninamaanisha utaondoka au kuamishwa. Leo kitabu chako cha kutoka kitaandikwa kwenye maisha yako. Wakoma walipoamua kutoka njaa waliiacha nyuma unapoamua kutoka ile hasara uliyokuwa unaiona hautoiona tena. My Lord my God,,,,,,,,, Ninaona watu wakitoka embu tuingie kwenye maombi ya kutoka, tumsii Mungu ili tuweze kutoka maana naona uweza wa Bwana unakutoa.

Mungu wangu tunaomba nguvu ya kutoka kwenye magonjwa yetu Bwana leo tunatoka kwenye shida Bwana, tunatoka kwenye umasikini Bwana. Historia zetu zinaandikwa upya kwa jina la Yesu. Leo ninatoka kwenye kukataliwa ee Bwana. Mungu wangu ninajua unalituma neno ili liweze kutuponya na sisi leo tunatoka kwa jina lako Bwana. Wewe Bwana unayefanya njia pasipo na njia leo tunatoka Bwana. Kama Mungu wetu uishivyo leo tunatoka Bwana, tunatoka Niko ambaye niko. Tunatoka leo Bwana na kukunguta mavumbi yote ambayo shetani alituvalisha kwa siku nyingi leo tunayakunguta kwa damu ya Yesu. Leo tunatoka kwenye shida zetu ee Farao mwenye moyo mgumu uliyetesa kwenye maisha yetu achia tutoke kwa Damu ya Yesu. Wewe uliyetutumikisha kwa muda mrefu leo tunatoka kwa Damu ya Yesu. Leo tunakupiga farao achia watu wa Mungu watoke kwa jina la Yesu.

Omba maombi ya kutoka kwenye kila vifungo na maonezi ya shetani kwa jina la Yesu.

Imeandikwa 1 Petro 1:18-19 Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; 19 bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.
Leo, ninatoka kwenye “(kumbukumbu zenu) database yenu” kwa damu ya Yesu kwa kuwa nimekombolewa kwa Damu ya Yesu.

Omba omba omba utaona matokeo yake   


Mungu akubariki na tuonane kesho tunaendelea na maombi ya siku ishirini na moja ikiwa ni siku ya nne leo. Na kwasababu kesho ni mapumziko tuwahi kwenye ibada ili tuweze kuwa na ibada nzuri Mungu akupe Neema ya kufika Amen.

No comments: