MUNGU WETU NI MOTO ULAO WAEBRANIA 12:29.

Wednesday, May 20, 2020

UMUHIMU WA KUKUA KIROHO



Mstari wa Kukumbuka 1Petro 2:2

Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;

KUUKULIA WOKOVU
Biblia inasema katika Yohana 3:6

Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.

Wewe sasa baada ya kutubu dhambi zako na kusamehewa, umezaliwa mara ya pili na ufalme wa MUNGU ni wako. Sasa basi tunapenda kuangalia jambo la muhimu sana, mtoto mchanga anapokuwa amezaliwa kwa mwili yaani katika hali ya kawaida ya kibinadamu, ili aendelee kuishi lazima apewe maziwa au siyo akiachwa tu hivyo atakufa. Vivyo hivyo na kilichozaliwa kwa Roho. Hiki nacho kinahitaji maziwa la! sivyo kitakufa hakika. Mtu baada ya kuzaliwa mara ya pili nilazima atamani maziwa ili aweze kukua, au siyo atadumaa na hatimaye kufa kiroho na kurudi kumtumikia Shetani, ili mtu aliyezaliwa mara ya pili aendelee na wokovu ni lazima anywe maziwa ya kiroho. Tunasoma katika 1 Wakorintho 3:1-2

 Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo.
Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi,

Baada tu ya kuzaliwa mara ya pili au kuokolewa, tunakuwa hatujui sana neno la haki, tunahitaji maziwa ili tuweze kukua na kukomaa katika wokovu.

Maziwa haya ni nini?
Maziwa haya ni kinywaji cha roho kinachotoka kwa Yesu Kristo ambacho ni Neno la Kristo, kama tunavyosoma katika 1Wakorintho 10:4

wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo.

Bila kupata mafundisho ya Neno la MUNGU mtu yoyote aliyezaliwa mara ya Pili lazima atadumaa, hatimaye kufa kiroho na kurudi tena katika utumwa wa dhambi. Hakuna uwezekano wowote wa mtu kuendelea katika wokovu bila kupata mafundisho ya Neno la MUNGU, hii ni kwasababu neno la MUNGU lina sehemu kubwa sana katika maisha ya kiroho (wokovu) ya mtu.


FAIDA ZA NENO LA MUNGU

NENO LA MUNGU NI CHAKULA CHA KIROHO

Mtu aliyeokoka hawezi kuishi kwa mkate tu wa kawaida. Siku zote mtu akikosa chakula mwili wake unadhoofika na kukosa nguvu, na mwili ukikosa nguvu mtu huyo hupoteza furaha yake. Mkate wa kawaida unaliwa na kuupa nguvu mwili tu. Mtu wa Rohoni yeye naye ni lazima apate Neno la MUNGU ili apate furaha na shangwe ya moyo wake tunasoma katika Yeremia 15:16.

Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana, Mungu wa majeshi.

Maneno ya MUNGU ni chakula halisi chenye uwezo wa kumkuza mtu kiroho na kumhakikishia uzima wa milele, Tukitaka kuishi milele ni lazima tulile Neno la MUNGU. Yohana 1:1; Ufunuo 19:13 Yohana 6:48-58. Tukiacha kulila Neno la MUNGU baada ya kuzaliwa mara ya pili, hatuwezi kuishi milele.  Chakula cha kawaida hata kiwe kizuri kama mana bado kitamfanya mtu afe na kuukosa uzima wa milele, baada ya kuokolewa hatuna budi kukipa uzito mkubwa chakula cha kiroho yaani neno la MUNGU ili tuishi milele na Yesu Kristo Mbinguni. tunasoma katika Yohana 6:48-49, 57-58

Mimi ndimi chakula cha uzima.
Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi.
Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele.
Tena tunasoma katika

Mathayo 4:4,
Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
Tunaona pia katika
Kumbukumbu la Torati 8:3

Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana.

Kwa maana mtu yoyote hata kama alipozaliwa mara ya pili, alipata badiliko kubwa namna gani? kukua kwake kiroho kunategemeana na chakula anachokula cha kiroho, au siyo atakufa kiroho hataendelea katika wokovu. MUNGU anakupenda mno kaka/Dada, ndiyo maana nakufundisha leo kuwa inakupidi upende mafundisho ya Neno la MUNGU kuliko hata chakula cha mwili. Watu wa MUNGU waliokuwa juu sana kiroho, wote walikuwa na tabia hiyo. Angalia mifano hii katika Biblia;
Ayubu 23:12
Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu,

Zaburi 119:72
Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu, Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.

NENO LA MUNGU NI TAA NA MWANGA WA NJIA YETU YA MBINGUNI

Njia ya mbinguni ni nyembamba sana, kwa maneno mengine imesonga mno; na mlango wa mbinguni ni mwembamba sana. Soma Mathayo 7:13; inatubidi wakati wote tuwe na taa na mwanga unaotumulikia mbele tuendako. Inafanishwa na mtu anayetembea wakati wa usiku juu ya daraja jembamba lililojengwa juu ya bahari. Bila mtu huyo kuwa na taa au mwanga, ni rahisi sana kuanguka baharini. Ulimwengu huu ni bahari ni njia pana. Yesu aliyetuokoa, ametuokoa kutoka katika bahari hiyo na kutuweka juu ya daraja jembamba. Kufika kwetu tunakokwenda kunategemeana sana jinsi tulivyon’gan’ania Neno la MUNGU ambalo ndio taa na mwanga wa njia. Tukiliacha neno la MUNGU ni dhahiri kabisa kwamba tutapoteza wokovu wetu na kuanguka tena baharini (Dhambini) au katika njia pana. Neno la MUNGU linasema katika Zaburi 119:105

Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu

Tunasoma pia katika Mithali 6:21-23

Yafunge hayo katika moyo wako daima; Jivike hayo shingoni mwako.
Uendapo yatakuongoza, ulalapo yatakulinda, Na uamkapo yatazungumza nawe.
Maana maagizo hayo ni taa, na sheria hiyo ni nuru, Na maonyo ya kumwadilisha mtu ni njia ya uzima.

NENO LA MUNGU NI SILAHA YA USHINDI JUU YA DHAMBI

Ni vigumu kabisa kuishinda dhambi bila Neno la MUNGU. Yesu Kristo katika Mathayo 4, alimshinda shetani alipokuja kumjaribu; kwa kulitumia Neno la MUNGU aliposema “imeandikwa” Hawezi kuishinda dhambi au majaribu ya Shetani.Ikiwa hupendi mafundisho ya neno la MUNGU, Shetani atakushinda tu. Dhambi itakushinda. Dhambi inawezwa na kushindwa na Neno la MUNGU pekee. Biblia inasema katika Zaburi 119:11
Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.

Kadri tunavyoisafisha njia yetu na kuifanya safi. Soma Zaburi 119:9 kwa maana nyingine ni kwamba maisha yetu ya kiroho yanafanywa safi kwa Neno laMUNGU. Yohana 15:3. Tukiacha kuyapenda na kuyafuata mafundisho ya Neno la MUNGU, tunaweza kufanya dhambi pasipokujua kwamba ni dhambi, na hilo bado linatufanya tuwe na hatia mbele za MUNGU. Neno la MUNGU linasema katika
Walawi 5:17

Na kama mtu akifanya dhambi, na kutenda mambo hayo mojawapo ambayo Bwana alizuilia yasifanywe, ajapokuwa hakuyajua, ni mwenye hatia vivyo, naye atachukua uovu wake.

Kwasababu hii, inatubidi tuwe tayari wakati wowote kuyafuata mafundisho ya neno la MUNGU, tusimtende Bwana wetu dhambi.

NENO LA MUNGU NI AFYA YA MIILI YETU NA NYUNDO YA KUYAVUNJA MATATIZO TULIYONAYO.

a)     Ikiwa tumepona baada ya maombezi katika mkutano wa Injili, au siku ya matendo ya ibada yoyote au maombezi, neno la MUNGU ndilo litakalo tuhakikishia uzima wakati wowote. Roho zetu zinapokuwa hazina neno la MUNGU na tunakazana kuzipamba kwa dhambi, Shetani yule aliyetutesa kwanza, hurudi tena na kututesa mara saba zaidi. Soma Luka 11:24-26. Hata kama hutujapokea uzima katika miili yetu ni lazima kufahamu dawa yamateso yetu ni neno la MUNGU. Tukizidi kulifuata ni lazima tutapata afya ya miili yetu. Mithali 4:20-22

Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote.
b)    Ukibanwa na matatizo yoyote, dawa siyo kuacha kuyatafuta mafundisho ya neno la MUNGU, ujue hiyo ndiyo nyundo ya kuyavunja matatizo yako yote yanayoonekana kwako kama mawe magumu. Neno hilo hilo ni moto wenye uwezo wa kuyateketeza matatizo hayo. Biblia inasema katika Yeremia 23:29
Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?

Ushindi wa shetani ni kukuzuia kupata chakula cha kiroho au Mafundisho ya Neno la Mungu

Mpaka hapa umefahamu Neno la MUNGU linafaida za ajabu, na ndilo litakalo kuwezesha kukua na kuishi milele. Sasa jambo muhimu la kuelewa hapa ni kwamba shetani naye anafahamu hivyo. shetani anakumbuka kwamba jinsi alivyoshindwa na neno la Mungu kule nyikani alipomjaribu Yesu, Mathayo 4:1-11. Kwasababu hiyo shetani atafanya kila linalowezekana kuhakikisha umekosa chakula cha kiroho au Neno la MUNGU ili “akuuwe” katika uchanga wako. Katika Biblia tunaona shetani alipopanga kumuua Yesu Kristo mara tu alipozaliwa, Mathayo 2:13,16. Sisi nasi tunapookolewa, tunakuwa tumezaliwa kwa Roho kama alivyozaliwa Yesu. Na Shetani tangia hapo anatafuta kila aliyeokolewa amuue. Mbinu kubwa anayoitumia shetani ili kumuua mtoto mchanga wa kiroho ni kumzuia kwa kila namna mafundisho ya Neno la MUNGU. Ukikosa mafundisho ya Neno la MUNGU unakuwa umekosa chakula cha Kiroho, na utadumaa na hatimaye kufa kabisa. Kwasababu hii Biblia inatuonya kwamba, Shetani asije akapata kutushinda kwa kukosa kuzijua hila zake. Soma 2Wakorintho 2:11. Sasa Basi ni makusudi ya somo hili, pia kukufahamisha namna mbali mbali atakazo tumia kukuzuia kupata chakula cha kiroho hivyo na kukuua. Ukizifahamu mbinu hizi za Shetani, basi usimpe nafasi Ibilisi kukuua. Mpinge naye atakukimbia. Soma Efeso 4:27 Yakobo4:7



NJIA TANO ANAZOTUMIA SHETANI KUMZUIA MTOTO MCHANGA WA KIROHO KUPATA NENO LA MUNGU NA HIVYO KUMUUA.

1.    Kumfanya ajione kuwa anajua na akatae kufundishwa.
Mtu yoyote akikosa ladha ya kula na akakata kula na akajisikia ameshiba hasikii kula, ujue maisha ya mtu huyo yako mashakani. Hii ndiyo mbinu shetani anayoitumia kumuua mtoto mchanga kiroho, kumfanya ajione hana haja ya kufundishwa. Ukitaka kupiga hatua kiroho ni lazima ukubali kwamba hujui lolote na ukubali kufundishwa Neno la MUNGU yafute yoyote unayofikiri kwamba unayajua. Angalia 1Wakorintho 8:2

Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua.

Watu wa Mungu waliofanikiwa katika Biblia na kufika ngazi ya juu ya kiroho, walikubali kuwa wajinga na hawajui neno na wakakubali kufundishika. Angalia maandiko katika Zaburi 73:22

Nalikuwa kama mjinga, sijui neno; Nalikuwa kama mnyama tu mbele zako.

Tena tunasoma katika Zaburi 143:10

Unifundishe kuyatenda mapenzi yako, Kwa maana ndiwe Mungu wangu; Roho yako mwema aniongoze kwenye nchi sawa,

Tukikubali kufundishwa ndipo tunapompendeza MUNGU na kuwa tayari kwenda kule aliko. Soma Zaburi 25:4-5 Yohana 6:45 Isaya 54:13. Kuangamizwa kwetu kunatokana na kukosa maarifa ya Neno la MUNGU. Tukikataa kufundishwa maarifa haya, MUNGU naye anasema atatukataa. Soma Hosea 4:6, kwasababu hiimpinge shetani katika eneo hili wakati wote naye atakukimbia. Kubali kujifunza Neno la MUNGU kanakwamba unaanza sasa, ukifanya hivyo ushindi wa kiroho ni kwako.
2.    Kusongwa na Shughuli za Dunia na udanganyifu wa mali
Mathayo 13:22

Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai.

Utaona tu mara baada ya kuokolewa shughuli za Dunia na kutafuta pesa zinakusonga kiasi kwamba masaa ishirini nne katika siku hazitoshi. Ujue huyo ni shetani aliyekuja kukuua. Ni kweli MUNGU anapenda tufanikiwe katika kazi zetu na Biashara zetu. 3Yohana 1:2 lakini ni lazima tuutafute ufalme wa MUNGU kwanza na hayo mengine yote tutazidishiwa. Soma Mathayo 6:33. Biblia inasema itamfaidia nini mtu akiupata ulimwengu na akapata hasara ya nafsi yake? Marko 8:36 Shughuli za Dunia na kutafuta mali hakikisha kwamba unafanya kwa wakati wake, wakati wa mafundisho ya Neno la MUNGU viache kwanza upate chakula cha roho yako ili kwamba usife. Shughuli za dunia zinazoweza kukuzuia usijifunze Neno la MUNGU zinaweza kuwa pamoja na matayarisho ya harusi mfululizo, wageni wanaokutembelea wakati wote, kuwatembelea ndugu, kuwaona marafiki, kuwatembelea wagonjwa n.k. Yote haya ni mema lakini kwa wakati wake. Biblia inasema katika Mhubiri 3:1kila jambo linawakati wake, wakati wa mafundisho ya neno la MUNGU uache kazi kabisa na ziache shughuli nyingine maana Neno ndilo uhai wako.

3.    Kumfanya mtu awe anatoa udhuru wakati wote anapohitajika kwenda kwa Yesu yaani kwenda kulisikia Neno la MUNGU
Utashangaa kwamba siku za mafundisho ya Neno la MUNGU ndiyo siku ambayo, litazuka mara hili mara lile, na utakuwa ni mtu aliyejaa udhuru, wakati wote. “Nisamehe, sikuweza kufika, kwasababu hii au ile” Ujue tayari umekwisha danganywa na adui Ibilisi, anataka ukose chakula na matokeo yake “ufe” Yesu akitoa mfano wa hali hii anasema katika Luka 14:16-20

Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa akaalika watu wengi,
akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njoni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari.
Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe.
Mwingine akasema, Nimenunua ng'ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe.
Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja.

Yesu anapotuita kumsikiliza, anataka tuache vyote tulivyo navyo na kumfuata. Huu ndiyo usalama wa Roho zetu Luka 14:33

Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

4.    Kumletea mtu dhiki na udhia kwa ajili ya wokovu aliopokea
Mathayo 13:20-21

Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha;
lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa.

Mbinu nyingine ya shetani baada ya wewe kuokolewa, ni kuleta dhiki udhia na mateso kupitia kwa ndugu zako. Anaweza akawa ni baba au mama, mumeo au mke wako., kaka au dada n.k. Nia ya dhiki hizi zinakupata ili ukate tamaa au uamue kutoendelea na wokovu kwa kuyasusia mafundisho ya Neno la MUNGU. Inakubidi uvumilie hadi mwisho hata kama ni dhiki za namna gani, usiliache Neno la MUNGU.MUNGU anasema ni heri kwa mtu wa namna hii. Soma Mathayo 5:11-12; 1Petro 4:12-16; Yakobo 5:10

5.    Kukufanya utafute mafundisho yaliyo karibu na nyumbani
hii tena ni njia ya shetani ya kukupeperusha mbali na chakula cha kiroho cha kukulia wokovu. Siyo kila kitu kilicho karibu ni cha MUNGU.MUNGU alichagua kuwapitisha wana wa Israel njia ndefu ya kwenda kanaani na kuiacha njia fupi. Soma Kutoka 13:17-18. Siyo kila mkesha au faragha iliyo karibu ni ya Mungu. Ni lazima uwe tayari kuifuata hekima ya MUNGU hata iwe mbali namna gani na gharama kiasi gani. Siku ya mwisho, malkia wa kusini atawekwa kuwa shahidi aliyefuata mafundisho mbali sana. Soma Mathayo 12:42 Ukitaka ukue kiroho uwe tayari kuwa kama Malkia huyu wa kusini.

Maziwa yasiyogoshiwa 1Petro 2:2
Maziwa yasiyogoshiwa ni maziwa halisi, safi yasiyochanganywa na maji au chochote. Maziwa haya ndiyo yanayomkuza mtu kiroho. Maziwa yasiyoghoshiwa ni Neno la MUNGUlililo thibitishwa na kuhakikiwa pasipo kuchanganywa na mapokeo ya wanadamu. Baada ya kuokolewa, siyo kila mafundisho ya Neno la MUNGU yanafaa kumkuza mtu kiroho ni lazima yawe mafundisho ya neno la MUNGU yasiyochanganywa na mapokeo ya wanadamu, mapokeo ya kidini yaliyoanzishwa na wanadamu yanapochanganywa na maziwa halisi yanakuwa ni sumu ya kumuua mtoto mchanga kiroho, au kumfanya adumae. Kwa sababu hii, ni lazima mafundisho yako ya kwanza katika wokovu yawe kweli ni mafundisho halisi ya Neno la MUNGU na siyo mafundisho tu ya kidini. Sasa wapi utayapata? lifuatalo ni jibu la swali hili.

Uchungu wa Mwana aujuae Mzazi Wagalatia 4:19-20
Umeokolewa na Bwana Yesu, hivyo wewe kama mtoto wa kiroho wa huduma hii, tunakusihi ukubali ikupe maziwa yasiyoghoshiwa ili ukue kiroho. Kwa nini umwache mzazi mapema hivi? Mafundisho yaliyoandaliwa kwa mpangilio maalumu ni muhimu sana kwa wewe kupiga hatua kiroho na kuukulia wokovu. Hivyo usikose ibada mbali mbali za wiki nzima katika kanisa la POWER OF GOD FIRE CHURCH. Ziko ibada nyingi nzuri, za aina tofauti tofauti katika kanisa hili. Ziko ibada za mikesha na maombezi kwa wagonjwa na wote wenye mahitaji mbali mbali. Siku ya Jumapili kuna mafundisho ya kina mapana na marefu, pamoja na kumsifu na kumwabudu Bwana, katika ibada ya siku ya Bwana. Usikose pia kujifunza masomo ya kwanza ya wokovu katika madarasa maalumu ya kuukulia wokovu ya Biblia

Kuja kwako kujifunza mafundisho haya ya kuukulia wokovu, siyo kubadilisha dhehebu lako la zamani. Makusudi ya mafundisho haya ni kuhakikisha umekuwa kiroho na uwe na msaada kwa watu wengine. Suala la wewe kujiunga na kanisa hili, ni hiari yako mwenyewe baada ya mafundisho hayo.

Wengi wamefaidika na mafundisho yaliondaliwa maalumu kwa mtu kuukulia wokovu, yanayotolewa na kanisa hili, ukihudhulia mfululizo baada ya muda Mfupi tu, utakuwa mwalimu wa wengine. MUNGU akubariki ukifanya hivyo, lakini mpinge shetani naye atakukimbia

MSAADA MWINGINE

A.    Kila siku tafuta Muda wa kujisomea Biblia
Kutafakari mafungu machache katika Biblia, kunaongeza kitu kikubwa katika maisha yako ya kiroho.

B.    Tenga muda wa Kumwomba Mungu asubuhi na usiku
Maombi ni mawasiliano kati ya mwanadamu na MUNGU. Zungumza naye kama Baba yako. Mweleze mahitaji yako. msifu kwa kukuokoa na mshukuru kwa yote anayokutendea. Mwombe akutie nguvu na kukushindia majaribu yote ili uendelee katika wokovu. Usisite kuomba kwa hofu kwamba hujui sana kuomba. Maombi ni mazungumzo kati ya mtoto na Baba yake. Zungumza na MUNGU kama unavyozungumza na Baba yako. Muda mfupi ujao baada ya mafundisho, utapiga hatua kubwa katika maombi. Usiofu kabisa, jipe moyo utashinda.











No comments: