MUNGU WETU NI MOTO ULAO WAEBRANIA 12:29.

Tuesday, February 19, 2019

NAMNA YA KUOMBA 2


 MAOMBI YA KUFANIKIWA NA MOYO ULIOTAYARI KUBEBA MAFANIKIO

Na Bishop Dankton Rudovick Rweikila 

Unaomba kufanikiwa lakini ndani yako hauko tayari kubeba majibu yako. Unaweza kuomba kweli lakini hauko tayari ndani ya moyo wako kubeba kile ambacho umeomba. Ni mtu mmoja anayeomba lakini ni huyo huyo ana moyo wa kupokea. Kuna nyakati nyingine watu wanaomba na kupewa majibu wakayakataa kwasababu ya ukubwa ma majibu uliyopewa. 

Mithali 3:5 
Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; 

Imani uliyonayo ndani ya moyo wako ndicho chombo cha kupokelea majibu yako. Unaweza kuomba kwa akili zako lakini ulichoomba kinapingana na Imani uliyobeba. Akili yako inahitaji nyumba, gari, shamba lakini imani yako inagoma. Unaweza kuwa ujanielewa vizuri, sikiliza ni pale unapokuwa unaomba lakini hauoni mazingira ya kulipata jambo hilo. Umeomba Biashara kwa maana ya uhitaji ulionao lakini Imani yako haiko tayari kupokea biashara uliyoomba. Unajitajidi kuangalia mazingira ya kupata biashara kampuni kwa kupitia akili yako lakini hauoni mahali pakupitia. Maandiko yanasema unapoomba unahitajika kuamini kwamba umepokea. Kuna tofauti ambayo ipo kumtegemea Mungu kwa moyo wako wote na kutegemea akili zako. Akili yako ina mipaka lakini ya Mungu haina mipaka ukiamini Mungu anaweza yanatokea. Ukitegema akili yako kuna mahali utafika na kukwama lakini ukitegemea Imani yako hakuna mahali ambapo utakamwa. 

Wana wa Israeli akili zao zilikwama lakini Imani zao hazikukwama na ndiyo maana walivuka bahari ya shamu. Hivi unadhani lilikuwa jambo jepesi kwa wao kuvuka bahari ya shamu wakati wanaangalia maji huku na kule. Inawezekana umeomba mafanikio halafu ukapewa bahari ya shamu na bado unaona kama haujajibiwa. Ni lazima uisogelee bahari ya shamu na haitafunguka kama haujasogelea bahari ya shamu. 

Kumbukumbu la torati 9:1-3

1 Sikiza, Ee Israeli; hivi leo unataka kuvuka Yordani uingie kwa kuwamiliki mataifa yaliyo makubwa, na yenye nguvu kukupita wewe, miji mikubwa iliyojengewa kuta hata mbinguni, 2 watu wakubwa, warefu, wana wa Waanaki, uwajuao, uliokuwa ukisikia wakitajwa hivi, Ni nani awezaye kusimama mbele ya wana wa Anaki? 3 Basi jua siku hii ya leo kuwa Bwana, Mungu wako, ndiye atanguliaye kuvuka mbele yako kama moto uteketezao; atawaangamiza, tena atawaangusha mbele yako; ndivyo utakavyowafukuza na kuwapoteza upesi, kama alivyokuambia Bwana. 


Kuna maombi ya kuvuka na kuna maombi ya kuinuliwa. Mungu anasema na wana wa Israeli mku tayari kuvuka kwenda kumiliki mataifa. Sikiliza Mungu anavyosema na wana wa Israeli kwamba mataifa hayo yana nguvu kuliko Israeli. Nisikilize nikuambie umasikini una nguvu kuliko wewe kama mwanadamu. Ndipo Mungu anasema usitumie akili yako bali umtegemee Mungu kwa akili zako zote na kwa moyo wako wote. 

Bwana anawauliza wana wa Israeli ni nani anayeweza kusimama juu ya wana wa Anaki? Maana yake ni nani anayeweza kusimama juu ya wachawi, majini au umasikini. Ukuta mrefu hupo na majitu yapo lakini Mungu anakutangulia. Kuna namna ambayo unatakiwa uangalie, uache kuona magonjwa umuangalie Mungu mbele yako. Mungu amewaonyesha wana wa Israeli kitu cha ajabu ambacho ukikiangalia kwa macho ya kawaida hauwezi kukiona. Mungu anaorodhesha kile ambacho wana wa Israeli watakutana nacho na kisha anawaambia yeye pekee ndiye atakayaweza kusimama mbele za wana wa Anaki. Mungu anawaambia wana wa Israeli atawaangamiza adui zao mbele yao. Kwa hiyo kama hauna Imani hauwezi kumuona Mungu akipigana na wana wa Anaki mbele zako. 

Imani ndiyo chombo cha kubeba majibu yako. Imani inabadilisha mazingira magumu kuwa mepesi, mazingira ambayo kibinadamu ni magumu kweli lakini Imani inabadilisha. Imani inaweza kubadilisha moto kuwa sehemu ya kukaa. Imani inaweza kukufanya uishi na simba kwenye shimo bila kupata madhara yeyote. Macho ya nyama yanaona uhalisia wa majitu, ukuta lakini Mungu anakuambia yuko mbele yako hiyo siyo hali ya kawaida. 

No comments: