MUNGU WETU NI MOTO ULAO WAEBRANIA 12:29.

Tuesday, February 19, 2019

KANUNI ZA MAJIBU YA MAOMBI


Na Pastor lambart Ileta 


Ufalme wa Mungu una kanuni zake na ukizijua kanuni zake na kuzifuata utafanikiwa, usipozijua utadhani Mungu hayupo. 

Kanuni ni kitu gani?

Ni muongozo unaoleta matokeo chanya. Ukifuata kanuni unaleta matokeo chanya na usipofuata hautaona matokeo. Tunaangalia kanuni za maombi kumbuka kwamba ufalme wa Mungu hauko hovyo hovyo. Inawezekana unataka majibu ya maombi yako lakini ni muhimu kujua namna ya kutumia kanuni. Sasa kabla hatujaenda mbali tuangalie maana ya maombi.

Maombi ni ushirika na maombi. Ninaposema ushirika maana yake ni kati ya pande mbili, siyo kwamba unaenda wewe na unaomba bila kumruhusu Mungu kusema na wewe. Unapoomba bila kupata majibu hayo si maombi. 

Mathayo 7:7-8
 Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. 

Unaona namna maombi yanavyoshirikisha pande mbili, kuna mtu ambaye anabisha na anafunguliwa anatafuta kisha anapewa. Kwa hiyo maombi si kupeleka jambo lako kiolela tu kwasababu Mungu majibu yako yote anayo. Kwa lugha nyingine tungesema maombi ni namna ya kupeleka haja zako mbele ya Mungu kulingana na neno lake. 

Yeremia 29:11 
Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. 

Mungu anayo tayari majibu ya maombi yako kwa hiyo ni kutafuta neno lake ambalo ndilo wazo la Mungu na kufananisha na mawazo yako. Siyo kwamba unapeleka mawazo yako binafsi mbele za Mungu hapana, unakwenda mbele za Bwana anayatoa kwenye akiba yake kisha anakupa majibu yako. Mungu siku zote anakuwazia mazuri na ya Amani mbele yako, kwa hiyo mawazo ya Mungu ndiyo sahihi kwako. 

Nini ambacho si maombi mbele za Bwana?
Ni malalamiko, uchungu, hasira na mambo kama hayo. Kanuni inayofuata baada ya kujua mapenzi ya Mungu ni kuondoa uchungu ndani yako. Maombi yako ya kilio uchungu na hasira hayambadilishi Mungu. 

Kuomba kwa manung’uniko na uchungu ni dhambi mbele za Mungu, haijalishi umetendewa jambo baya kiasi gani. 

1 Wakorintho 10: 10
Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu. 
Haijalishi una uchungu kiasi gani Mungu anahitaji uende mbele zake kwa hoja. Hata kama una maadui wengi kiasi gani kuna namna ya kupeleka hoja mbele za Bwana. Si wakati wako wa kulia.

Isaya 49:26
Na hao wanaokuonea nitawalisha nyama yao wenyewe, nao watalewa kwa kuinywa damu yao wenyewe, kama kwa mvinyo mpya; na wote wenye mwili watajua ya kuwa mimi, Bwana, ni mwokozi wako, na Mkombozi wako ni Mwenye enzi wa Yakobo.

Wanafunzi wa Yesu walimuambia Yesu tufundishe namna ya kusali na Yesu akawafundisha sala ambayo imejaa kanuni zake zote za namna ya kuomba. 

Mathayo 6:9 
Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, 10 Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni. 11 Utupe leo riziki yetu. 12 Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. 13 Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.] 


Kwanza lazima useme Baba yetu uliye mbinguni, Mungu si wa wote na shetani si wa wote. Kabla ya kusema Baba yetu uliye mbinguni lazima kwanza ujiangalie nastahili kumuita Baba na je nikimuita hatasikia. Mungu si Baba wa kila mtu kama ambavyo wewe si Baba wa kila mtu. Wewe ni mtu wa Mungu kwa maana alikuumba yeye lakini unaweza usiwe mtoto wake kwasababu ya mahusiano yako na yeye. Wako wanaostahili kumuita Baba maana yake wale waliookoka na kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu. Kwa hiyo kuna vitu vya kukamilisha pamoja na kuoka lakini vipo vya kukamilisha. Maandiko yako wazi kabisa katika ili kwa mujibu wa maandiko yanasema si wote Mungu si Baba wa wote. Maandiko yanasema ni wale waliookoka na kubatizwa na kupokea nguvu ya Roho Mtakatifu. Wakati unaongelea kwa habari ya Baba na mwana hauwezi kumuacha Roho Makatifu. Nilimfurahia Nikodemo aliuliza swali zuri sana tusome; 

Yohana 3:1-31 Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi. 2 Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye. 3 Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. 4 Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? 5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. 

Sasa jiulize swali moja hapa, kama mtu hawezi kuingia kwenye ufalme wa Mungu kwasababu hakuzaliwa mara ya pili anawezaje kumuita Mungu Baba na akaitika. Yesu anamuambia wazi Nikodemo kwamba mtu asipozaliwa kwa maji na Roho hawezi kuingia ufalme wa Mungu. Ndiyo maana ni muhimu kujua je ulipobatizwa ulipokea Roho Mtakatifu. 

Yesu alipomuendea Yohana kwaajili ya kubatizwa baada ya miaka thelathini ya kuzaliwa kwake Yohana alikataa kumbatiza na kumuambia yafaa yeye ndiyo abatizwe naye. Lakini Yesu alisema “Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali” 

Ngoja tuangalie wale wanaostahili kumuita Mungu Baba ni watu gani tusome Warumi 8:14-15
14 Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. 15 Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. 

Kama unaye Roho umeokoka na kubatizwa unaenda kwa Mungu na uhakika, kwa maana haujapokea Roho ya utumwa. Unaenda kuongea na Baba yako ili umkumbushe kwamba Baba umesema hivi kwenye neno lako na mimi naomba hili na lile. Hii ni hatua ya kwanza ya Baba yetu uliye mbinguni. 

Kwa hiyo hatua ya pili ni kumtukuza Mungu wako, maandiko yanasema Mungu anaketi kwenye sifa anaposifu unampa sifa Baba yako aketi ili akusikilize shida yako. Mungu lazima umtukuze kwa majina yake, ukuu wake, na enzi yake. Ndipo Mungu anakuja kuketi na kukusikiiza unasema nini ili apate kukujibu. Unaposema ufalme wake uje hapa Duniani ni lazima ujue kwamba ufalme wake unakujaje. Maana yake kuna watu wanauleta ule ufalme wa Mungu hapa Duniani. 

Mathayo 6:33 
 Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. 

Mapenzi yako yatimizwe 

Yohana 15:7 
Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. 


Tupe leo Riziki zetu hapa ndipo mahali pa kumwaga sera zako zote kwa Mungu. Omba bila shaka na hitaji lako utapata. Usiombe kulingana na mazingira yako, usiombe mtaji kwa Mungu kisha ukamfikiria kaka hapo siyo Mungu tena ni kaka. Usiangalie mazingira yako Mungu anatenda kwa uweza wake kwa njia anayoijua yeye. 

Ufunuo 5:12
wakisema kwa sauti kuu, Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka. 

Kanuni ya Sita utusamehe makosa yetu 

Usitutie majaribuni
Mungu hawezi kumjaribu mwanadamu kwa hiyo tunajaribiwa na tamaa zetu wenyewe 

Kwa kuwa ufalme ni wako na nguvu na utukufu. Ukimaliza kuomba unamshukuru Mungu kwa kukujibu maombi yako sawa sawa na neno lake. 


No comments: