Na Pastor Lambart Ileta
Mungu ni Mungu ambaye anapenda watoto wake. Na unapoomba inakupasa kuamini kwamba atajibu. Siku zote maombi au majibu ya maombi ni mchakato. mambo mengine ni lazima yafanyiwe mchakato ingawa mengine Mungu anaweza kujibu papo kwa papo inategemeana na dharura iliyopo. Kama vile ambavyo wewe Baba unaweza kumpa mtoto wako kitu anachokuomba hapo kwa hapo au kuna mengine unafanyia mchakato ili kuweza kumtimizia mwanao.
Unapomuomba Mungu anajibu na inategemeana na dharura uliyonayo kwa muda huo. Kwa hiyo kama unadharura Mungu anaingilia kati wakati huo huo na unapata majibu lakini kama sivyo basi majibu yako yanajibiwa kwa wakati wake. Shida yetu sisi tunaona Mungu ajajibu maombi yetu au hajibu maombi yetu.
Isaya 49:13-15 Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. 16 Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima. 17 Watoto wako wafanya haraka, hao wakuharibuo, nao waliokufanya ukiwa, watatoka kwako. 18 Inua macho yako, ukatazame pande zote; hao wote wanajikusanya na kukujia. Kama niishivyo, asema Bwana, hakika utajivika na hao wote, kama kwa uzuri, nawe utajifungia hao, kama bibi arusi. 19 Maana katika habari za mahali pako palipokuwa ukiwa, pasipokaliwa na watu, na nchi yako iliyoharibika hakika sasa utakuwa mwembamba usiwatoshe wenyeji wako, nao waliokumeza watakuwa mbali. 20 Watoto ulionyang'anywa watasema masikioni mwako, Mahali hapa ni pembamba, hapanitoshi; nipe nafasi nipate kukaa.
Mungu anasema hatawahurumia watu wake walioteswa hivyo kama umeomba muda mrefu jua kwamba Bwana amesikia na amekuhurumia. Sayuni aliomba kwa muda mrefu na hakuona Mungu akitenda kama vile ambavyo yeye ametaka. Huenda alifunga na kufunga na hakuona majibu na hakaona kama Yehova amemuacha. Watu wengi sana wanapoomba na kuona kwamba wamechukua muda kwenye maombi ndipo wanaanza kulaumu kwasababu ya haraka ya kujibiwa na kuona kwamba Mungu ni wambali. Sikiliza nikuambie Mungu si wambali ni Mungu wa Karibu.
Unakumbuka kuna wakati tulisoma juu ya Yusufu na KIBALI tukaona namna Yusufu alivyokuwa kijana mdogo na jinsi alivyoweza kutimiza ndoto yake. Yusufu ameota ndoto akiwa na miaka 17 lakini akiwa na miaka 30 ndipo ndoto yake inatimia miaka kumi na mitatu baadae, kwa hiyo ilikuwa ni hatua ya kimchakato mpaka Yusufu kufikia ndoto yake. Mtazame Daudi amepakwa mafuta akiwa kijana mdogo tena mafuta ya kifalme lakini alikuja kuwa mfalme takribani miaka 33 baadae. Daudi hakukata tamaa kuna wakati alikosa chakula kuna wakati alikuwa na vita kali sana lakini alikuwa na mafuta ya kifalme aliyopakwa na nabii Samweli.
Sasa Sayuni analia na kuona kama Mungu amemsahau katika maombi yake.
Kwanini Majibu yako yanachelewa?
Ukisoma Biblia kuna sababu kadhaa za majibu yako kutojibiwa. Inawezekana kuna mtu ameshikilia majibu yako hivyo kuna hatua nyingine za kuchukua ili majibu yako yapatikane
Sabubu zinaweza kuwa ni;
Mungu anasema " Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe”Kwa hiyo inawezekana mama kumsahau mwana wa tumbo lake lakini Mungu hawezi kukusahau wewe. Na Mungu leo hakukumbuke kwa jina la Yesu na hayakumbuke maombi yako kwa jina la Yesu.
Mungu anaonyesha namna ya kujibu mambi yako lakini anasema watoto wako wanafanya haraka. Mungu anaanza kuonyesha mchakato wa maombi kuanzia mstari kumi na saba.
Kuna watu wengine wameomba na kutendewa lakini Shetani amewapiga upofu wanalalamika. Ukimuangalia na kumuuliza unaona lipo jambo ambalo Mungu amelitenda kwenye maisha yake lakini yeye haoni kama ametendewa. Mungu akufungue macho yako na ukaone majibu yako kwenye ulimwengu wa Roho kwa jina la Yesu. Utakuta mtu anasema sina hela na ukimuuliza anajilinganisha na nani kuwa ana pesa hauwezi kupata majibu. Wengine utakuta wakisema mimi naumwa lakini ukimuuliza anajifananisha na nani hana majibu.
Maandiko yanasema pale palipo ukiwa patajaa mpaka mahali hapo pawe pembamba hata kusitoshe tena na wale waliokumeza watakuwa watakuwa mbali. Mchakato wa Mungu ni lazima kwanza amuondoe adui yako ndipo wewe uweze kustawi kwasababu hauwezi kustawi kama bado adui amemeza mali zako. Unaweza kupata fedha kidogo lakini isionekane yupo anayemeza kwa hiyo ni lazima atapike na akatiliwe mbali ili uweze kustawi kwa jina la Yesu. Baraka za Mungu siyo za majuto kwa hiyo Mungu anahitaji kuona unastawi na anapoachilia kitu kwako hataki kimezwe na adui yako.
“20 Watoto ulionyang'anywa watasema masikioni mwako, Mahali hapa ni pembamba, hapanitoshi; nipe nafasi nipate kukaa.”
Mungu anapokubariki hata mahali unapokaa hapatatosha na ndipo utakapohitaji kupanuka kwasababu ya wingi wa Baraka hizo. Kuna mambo ambayo yatatokea na utaanza kujiuliza ni mimi kweli ambaye yamenitokea kwasababu ya ukuu wa majibu ya Mungu.
22 Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, nitawainulia mataifa mkono wangu, na kuwatwekea kabila za watu bendera yangu; nao wataleta wana wako vifuani mwao, na binti zako watachukuliwa mabegani mwao.
Bwana akishainua bendera yake juu ni wakati wa ukombozi na wale walioteka mali zako watazileta kwa heshimu wakiwa wamezibeba na binti zako wataletwa mabegani kwa heshima kubwa. Kwa hiyo hawatarejesha katika hali ya kawaida bali kwa heshima. Ni muhimu sana kutambua kwamba Mungu wako yupo usitange tange hovyo na kukimbia, kama vile Israeli waliondoka kwa heshima hawakuondoka bila kitu. Tunaona Esta namna ambavyo Mfalme alimuambia Malkia sema hata nusu ya Ufalme wangu nitakupa Esta anamtuliza mfalme wala hakusema bali anatulia na kutaka mfalme aende karamuni. Lazima Heshima ya Mungu ionekane.
23 Na wafalme watakuwa baba zako za kulea, na malkia zao mama zako za kulea; watainama mbele yako kifudifudi, na kuramba mavumbi ya miguu yako; nawe utajua ya kuwa mimi ni Bwana, tena waningojeao hawatatahayarika.
Maandiko yanaseam wafalme ndiyo watakuwa Baba zao wa kulea. Mungu hawezi kukupa ajira na akakosa kukupa wafanyakazi kwenye ajira hiyo. Si unakumbuka Musa namna ambavyo Musa aliandaliwa maalumu kwaajili ya wana wa Israeli japo kulikuwa na amri juu ya watoto wote wa kiume wa Waebrania wauwawe. Musa anawekwa kwenye kisafina na anakwenda kulelewa na Binti Farao ikulu ya Misri na mama yake ndiye anamelela tena kwa kulipwa. Yule aliyetafutwa kuuwawa akatupwa kwenye maji na anapelekwa mbele ya adui yake ambaye ni mfalme kumlelea na bado mama anapata ujira kuna jambo kubwa kama hilo. Waliokutesa watalamba mavumbi ya miguu yako na watasema hakika huyu ni Mungu aliye hai. Hiyo ndiyo heshima ya mwana wa Mungu ndiyo maana anaposema sijakusahau anamaana kubwa sana, ila wewe tu haujajua mpango wa Mungu kwenye maisha yako. Mungu anakuwazia yaliyo mema siku zote za maisha yako.
Tamani sana maombi ya Muda mrefu maana ndiyo nguzo ya majibu ya maombi yako.
No comments:
Post a Comment