MUNGU WETU NI MOTO ULAO WAEBRANIA 12:29.

Tuesday, February 19, 2019

Somo la Kwanza


HAKIKA UMEOKOLEWA

Mstari wa kukumbuka Zaburi 103:12
“Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi”

UHAKIKA WA WOKOVU

Moja ya mbinu kadha za shetani za kuwarudisha nyuma watu waliokata shauri kuokoka, katika uchanga wao, ni kuwafanya wawe na mashaka kwamba wameokoka. Wawe na mashaka kwamba wamesamehewa kabisa dhambi zao. Mbimu hii itatumika pia kwako, na huenda mpaka sasa umepata mawazo ya namna hii, “wewe kweli umeokoka auunajidanganya mwenyewe?” “Mbona hakuna badiliko lolote, uko vilevile?” Mbona umekasirika leo asubuhi na watu waliookoka hawapaswi kuwa na hasira? Tunapokea wokovu kwa Imani sio kwa hisia au kwa kujisikia kwambatumeokoka. Mwili wetu utakuwa vile vile na hakuna badiliko la mwili linaloonekana, lakini katika Roho kuna mabadiliko makubwa yanayokuwa yametokea. Mambo ya kiroho yanatambulika kwa jinsi ambavyo tunasoma neno la MUNGU na siyo hisia zetu. Hata kama rafiki zako wangekusuta asubuhi, na kukuambia wewe haujaokoka mbona umesema lile na umefanya lile, hayo yasikutoe katika mstari na kukutia mashaka juu ya wokovu wako ulioupokea. Angalia tu Neno la Mungu linasema nini usiyaruhusu mashaka. Mashaka au wasiwasi maneno hayo hayatoki kwa MUNGU, na hivyo hayatakiwikukutawala na kukupotosha. Mashaka na wasiwasi vyote hutokana na adui Ibilisi. Mtoto hazaliwi na kuwa mtu mzima kwa siku moja.

Vivyo hivyo na mtoto wa kiroho. Sasabasi, Neno la Mungu linasema nini juu yako baada ya kukata shauri? Paleulipojingundua kwamba wewe ulikuwa ni mwenye dhambi kwa kuzaliwa mara ya pili, na kuzijutia dhambi zako kabisa, na kuamini kwamba Kufa kwa Yesu msalabani ndiyo kulikuwa upatanisho kati yako na MUNGU na ukatubu dhambi zako na kuwa tayari kuziacha kabisa, mambo kadhaa yametokea kiroho katika tendo hilo.
1)   Dhambi zako zimesamehewa, na Mungu hazikumbuki tena.
Mtu yeyote anayetubu kwa dhati dhambi zake na kuwa tayari kuziacha dhambi hizo, mtu huyu dhambi zake zimesamehewa kabisa na hazitakumbukwa tena na MUNGU. Tunaona haya katika Zaburi 103 :12,

Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.

Isaya 43:25 
Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.

Wakolosai 1:13-14;21-22  
Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;
ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;
Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa;
katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama;

WEWE SASA UNA UZIMA WA MILELE.
Kabla ya kutubu dhambi zako na kuziacha kwa kumwamini Yesu Kristo Mwana wa MUNGU aliyekufa kwaajili ya Dhambi zetu, wewe ulikuwa katika ghadabu ya MUNGU na uzima wa milele ulikuwa mbali na wewe.  Wewe ulikuwa mtu wa kwenda Jehanamu. Ulikuwa Chini ya Hukumu. Sasa hauko tena chini ya hukumu, uzima wa milele ni wako. Nyumbani kwako sasa ni Mbinguni alipo mwokozi wako Yesu Kristo. Tunaona haya katika Yohana 3:18 ,3:36 1 Yohana 5:11-13
Yohana 3:18
Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu

Yohana 3:36                                                                  Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia.

1 Yohana 5:11-13
Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe.
Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima.
Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu.

HUTAPOTEA KAMWE UKIWA MIKONONI MWA YESU

Kuanzia ulipokata shauri kuokoka, wewe sasa uko mikononi mwa Yesu Kristo na yeye nia yake na mapenzi yake kabisa ni kwamba, uende mbinguni huko alipo na kufurahi nae milele na milele. Mapenzi ya MUNGU Baba naye ni hivyo hivyo kwa kuwa yeye ni mwenye nguvu kuliko Shetani na yeyote yule, basi atahakikisha kwamba yeyote atakaye taka kukupokonya mikononi mwake na kukupoteza ili urudi kwenye ghadhabu ya milele hatafanikiwa. Hivyo ndiyo ahadi yake kwako. Hata hivyo wewe una sehemu ya kufanya ili haya yatimie kwako, inakubidi kufanya mambo, yafuatayo kuanzia sasa: -

        I.        Uisikie sauti ya Yesu
Sauti ya Yesu ni Neno la MUNGU. Inakubidi kila utakalojifunza katika Neno la MUNGU yaani biblia ulisikia na kuliweka moyoni. Nilazima upende kusikia neno la MUNGU, upende kulisoma neno la MUNGU, upende pia kujifunza neno la MUNGU.


      II.        Umfuate Yesu
Yesu ni mtii na kondoo wake inawapasa kuwa watii pia, ukisikia neno la MUNGU linasema ubadilike, basi inabidi uwe mtii na kumfuata Yesu. Jambo lile analolitaka Yesu ulifanye katika Neno lake, basi lifanye mara moja. 
Huko ndiko kumfuata Yesu. Usijiongoze mwenyewe katika jambo lolote. Yafuate maongozi ya Yesu ndiye mwokozi wako, lakini pia ni Bwana wako ni lazima ukubali awe dereva wakoZaburi 16:11. Hapo mwanzoulikuwa unafanya unalolitaka tu sasa unafanya analolitaka Bwana wako.

Popote Yesu anapokupeleka katika Neno la MUNGU, basi na wewe mfuate huko. Mtu anayekataa kumfuata Bwana wake huyo ni makaidi na muasi. Wewe umeokolewa katika uasi, maana dhambi ni uasi 1Yohana 3:4hivyo hupaswi kumuasi tena Bwana wako. Ukifanya haya, hakuna yeyote wa kukupokonya uzima wako wa milele uliopokea. Kuanzia sasa makao yako, yapo mbinguni. Yohana 10:27-29,
Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata.
Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu.
Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu.

JE, UKIFANYA DHAMBI HUTAPOTEA?

Dhambi ni kitu cha kukichukia kabisa. Hata hivyo mtu aliyeokoka bado anaweza akawa anatenda dhambi. Unachotakiwa kufanya unapogundua kuwa umetenda dhambi ni kutubu dhambi hiyo kwa MUNGU mara moja na kuiacha. Usidanganyike kwamba kwakuwa umetenda dhambi sasa hakuna wokovu tena kwako. Hapana! Hakika yako ya wokovu iko pale pale. Jambo muhimu tu ni kwamba unapogundua kwamba umetenda dhambi unatubu na kuiacha.

Hata hivyo, mtu aliyeokoka hawezi kufanya dhambi kwa kukusudia!
Anajua hili ni dhambi halafu analifanya kwa makusudi, eti halafu atatubu! Mtu wa jinsi hiyo bado yuko gizani kabisa, hajaokolewa. Mtu aliyeokolewa anachukia dhambi na akijikuta amefanya dhambi, anahuzunika na kutubu maana tumeitwa katika utakatifu. Katika hatua za mwanzo za wokovu unaweza ukajikuta unaanguka hapa na pale mara kwa mara lakini inakubidi utubu na kuiacha.
1 Yohana 2:1-2,
Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki,
naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.”

Waefeso 1:4-5
kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo.
Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.
Hivyo fahamu bila shaka wewe umeokoka na uzima wa milele ni wako. Sema Bwana asifiwe kwa Furaha ya wokovu. Neno la MUNGU linasema katika Wafilipi 1:6 

Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu;

-->

No comments: