MUNGU WETU NI MOTO ULAO WAEBRANIA 12:29.

Wednesday, July 21, 2010

MAPENZI YA KWELI


Usiutese moyo wako kwa mwanamke asiye na mapenzi ya kweli!





.Wengi huingia katika uhusiano baada ya kuwa na mapenzi ya kweli na wenzi wao, lakini wakati mwingine unaweza kuwa katika uhusiano na mpenzi unayempenda, lakini kwa bahati mbaya akawa hakupendi au ukashangaa anazidisha vituko kila kukicha.



Leo nazungumzia upande mmoja (wanaume), ingawa maumivu ya mapenzi kwa upande wa wanaume ni tofauti kidogo na wanawake lakini wapo wanaume wengi ambao wapo katika uhusiano uliopoteza dira na hawajui kitu cha kufanya.



Wanashindwa kuelewa kuwa wao ndiyo wenye makosa au wapenzi wao ndio ambao hawana mapenzi ya kweli. Katika hili wengi hushindwa kutoa maamuzi (kuachana) wakiamini huenda wakawa wameamua vibaya kwakuwa labda wenzi wao wanawapenda ila kuna matatizo ya hapa na pale.



Hilo lina msingi kidogo, lakini unaweza kung’ang’ania penzi la mwenzi ambaye hana dira mwisho wa siku ukaishia kuumizwa huku akilini mwako ukibakiwa na neno ‘laiti ningejua’, wakati huo utakuwa umeshachelewa! Vipengele vifuatavyo ikiwa utavisoma kwa umakini, kwa maana ya kujifunza mambo na kuelewa, utapata maarifa mapya katika uafahamu wako juu ya uhusiano na mapenzi. Hebu vipitie...



HESHIMA HUANZA KUPUNGUA...

Hili lazima uwe nalo makini sana unapomchunguza mwenzi wako, mwanamke mwenye mapenzi ya kweli lazima atakujali na kukuheshimu, asiyekupenda huwa hachagui jibu la kukupa!

Kwa bahati nzuri kipengele hiki ni rahisi sana kung’amua, utaona majibu yake yanavyokuwa mabaya, haogopi kitu chochote, hahofii adhabu au kukupoteza. Inawezekana kabisa ukamwambia kitu chenye mantiki lakini akawa mgumu kukuelewa.


Swali la kujuliza hapa ni je, mwanzoni alikuwa na tabia hizi? Maana kuna wanawake wengine wana asili ya ukorofi, lakini kama hakuwa na tabia hizi, basi fahamu kuwa nafasi yako imekwisha, huna sababu ya kuendelea kuumia maana mwisho wa siku atakuumiza zaidi atakapokaumbia hakutaki. Ni bora ukaachana naye mapema kabla ya kukuumiza zaidi wewe.



HAKUTHAMINI...

Hili nalo ni tatizo kwa mwanamke wa aina ninayoizungumza, mwanamke ambaye hakupendi huwa na wewe kwa ajili ya maslahi yake na siyo mapenzi. Ikiwa utapata matatizo ya kikazi au kupatwa na msongo wa mawazo kutokana na migongano ya kimaisha, hawezi kutoa msaada wa mawazo kwako. Atachukulia tatizo lako kama lako mwenyewe, lakini mwanamke ambaye anakupenda huwa karibu na wewe, hukupa moyo na kukusaidia kwa hali na mali.



Kadhalika hawezi kukusaidia unapokuwa mgonjwa, hakujali tena kwa kuwa kile alichokuwa akikipata kwako hatakipata tena, unaweza ukaumwa ghafla lakini yeye hatajali na wakati mwingine hata kukujulia hali kwa njia ya simu pia humuwia vigumu.




Mbaya zaidi ni pale utakapofukuzwa kazi, sio ajabu ikawa ndio mwisho wa mapenzi yenu! Lakini ili kuwa na uhakika zaidi juu ya hili, mpe mtihani, jifanye unaumwa uone mwenzi wako anakuwa karibu na wewe kiasi gani, lakini pia ili uweze kuwa na uhakika zaidi, jifanye umefukuzwa kazi! Ataendelea kuonyesha mapenzi au ndio atakimbia? Huo utakuwa mtihani unaomfaa sana mpenzi ambaye una wasiwasi naye.

SILAHA YAKE NI NGONO



Mwanamke wa aina hii huamini ngono ndio kila kitu, yaani ni sawa na mapenzi yenyewe, kwa maana hiyo hutumia kitendo cha ngono kama silaha yake ya mwisho! Mathalani kama akihitaji fedha au kitu cha gharama, kama utashindwa kufanya hivyo kutokana na muingiliano wa ratiba zako kifedha, hutishia kukunyima penzi!




Anaamini kuwa penzi ni silaha yake ya mwisho katika kukufanyia ‘usanii’ wake wa kujidai anakupenda wakati ukweli halisi haupo hivyo. Inawezekana ukawa upo naye nyumbani kwako au mahali popote kwa nia ya kufurahia mapenzi pamoja lakini akiona dalili kuwa huna pesa basi hutishia kukunyima penzi.



Mwanamke wa aina hii anapenda ‘pochi’ lako na sio wewe, hata ukiumwa au kutetereka kidogo kifedha huenda akaachana na wewe! Kwa sababu hakupendi wewe, anapenda pesa zako, sasa kama zimeisha anasubiri nini kwako? Mwanamke wa aina hii ni sumu ya maendeleo yako. Je, kuna sababu ya kuendelea kuwa naye? Hakika hakuna.

1 comment:

Mike Manuel said...

nimekukubali japo nimepita juujuuu sana. bwana mdogo uko vizuri kwenye hii sekta.

big up man.